Maoni: Hukumu ya Radovan Karadzic ni sawa kabisa
21 Machi 2019Hizo ni habari njema kwa wote wale wanaotaka kuona kwamba maovu ya mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu yanafuatiliwa mbali duniani kote na wanaoyatenda wanachukuliwa hatua za kisheria.
Radovan Karadzic aliyekuwa kiongozi wa Serbia wakati wa vita vya nchini Bosnia-Herzegovina iliyokuwa sehemu ya Yugoslavia atayamalizia maisha yake jela. Hiyo ni hukumu iliyotolewa na mahakama ya mjini The Hague baada mahakama hiyo kuitupilia mbalirufani yake baada ya hapo awali kupatikana na hatia ya kutenda uhalifu katika vita hivyo kati ya mwaka 1992 na 1995.
Karadzic anatambulika kwa ukatili wa kuwaandama na kuwatimua raia waliojitokeza kupinga sera za siasa kali za Waserbia na hasa ukatili waliotendewa raia ambao hawakuwa waserbia kutoka sehemu za Bosnia ambazo hazikuwapo chini ya udhibiti wa majeshi ya ya Karadzic.
Karadzic alitumia mkakati wa kuyazingira maeneo ambako wazalendo wa kiserbia hawakuweza kuyadhibiti.Kutokana na mkakati huo watu zaidi ya 11,000 waliuwawa katika mji mkuu Sarajevo pekee, ikiwa pamoja miongoni mwao wanawake na watoto.
Unyama wa Karadzic ulifikia kilele baada ya majeshi yake kuuteka mji mdogo wa Sebrenica wa mashariki mwa Bosnia. Wanajeshi wa Karadzic waliwaangamiza waislamu 8000, vijana na watu wazima lakini baada ya muda mfupi majeshi ya NATO yaliingilia kati na kuvimaliza vita vya Bosnia.
Kutokana na shinikizo la kimataifa Karadzic alikimbia na kujificha. Licha ya majeshi ya kimataifa yaliyokuwa yamewekwa Bosnia kumtafuta, Karadzic aliweza kujibanza kwa muda wa miaka 10 katika nchi jirani ya Serbia. Alikamatwa mnamo mwaka 2008 wakati akijifanya mganga. Alifikishwa mbele ya mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague na mnamo mwaka 2016 alihukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka 40 jela lakini aliazimia kukata rufani kwa sababu baadhi ya masuala fulani hayakuzingatiwa katika kesi lakini hakufanikiwa.
Mahakama imethibitisha hukumu ya hapo awali ilikuwa sahihi na imeongeza adhabu ya kifungo cha maisha jela. Hukumu hiyo imetoa ujumbe kwa wale wenye itikadi kali za kizalendo nchini Bosnia na pia ni ujumbe kwa wale wanaoikosoa mahakama ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia uhalifu uliotendwa katika Yugoslavia ya zamani.
Pia ni ujumbe kwa nchi kama Marekani, Urusi na China zinazopinga kuwapeleka wananchi wao kwenye mahakama za kimataifa ili kuhukumiwa. Mahakama ya kimataifa mjini The Hague imethibitisha kwamba inao uwezo wa kutoa haki licha ya upinzani uliopo.
Vyanzo: http://www.dw.com/a-47997547