1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Imarisha ulinzi, bali usichanganyikiwe

Volker Wegner/Mohammed Khelef19 Novemba 2015

Ugaidi hausambazwi kwa bunduki za Kalashnikov na mabomu pekee, bali pia kisaikolojia kupitia khofu miongoni mwa watu, lakini khofu hiyo inaweza kukabiliwa kama anavyoandika Volker Wagener wa DW.

https://p.dw.com/p/1H8jN
Frankreich Schießerei bei Polizeiaktion in Saint-Denis Paris
Picha: picture-alliance/dpa/MASPPP

Mjadala huu ulitazamiwa: Je, twende kwenye masoko ya Krismasi mwaka huu? Wanafamilia wanajiuliza wakiwa wamezunguka meza za chakula majumbani mwao. Kwa sasa, mama wana jawabu kubwa la HAPANA. "Haifai kwenda mwaka huu. Ni hatari sana. Na watoto bila ya shaka hawendi popote." Wanaume - wawe mababa ama la - huwa wanajifanya kutulia na kutumia hoja, wakichukuwa msemo kuwa: "hakuna aliye salama zaidi kuliko aliye sahihi baada ya mashambulizi."

Mijadala kama hii inajenga taswira moja: jinamizi la ugaidi limekuwa halikwepeki. Khofu inazozitengeneza zinanyizofoa nyoyo zetu na hata akili zetu pia. Je, bado naweza kuhudhuria tamasha la muziki au mechi ya mpira wa miguu? Kwa kiasi gani shule zetu ziko salama? Je, bado ni salama kupanda treni? Je, sherehe za kanivali zitakwenda kama zilivyopangwa?

Volker Wagener
Volker Wagener

Khofu zinaweza kuzuiwa kuwa wazimu

Khofu hizi zinaweza kuelezeka kama sio kuhalalishika. Pamoja na hayo, kabla hazijageuka kuwa wazimu kamili, lazima tuzizuwie, na kuvuta upumzi mzito. Ni kweli, adui huyu haonekani, haandamani mitaani ili tuweze kumuoteza kidole, ni yule. Huwa tu tunamjuwa kuwepo kwake wakati tukiwa tumeshachelewa, baada ya majeruhi kwishatenganishwa na maiti. Lakini tunaweza kupata suluhisho gani?

Uimarishaji wa usalama hauepukiki. Kwa muda mrefu, tumekuwa tukichukulia ni jambo linalokubalika kupunguza idadi ya polisi ili kupunguza matumizi ya fedha, kwani hilo ndilo la kupewa kipaumbele. Ajira nyingi za wanausalama zimepunguzwa, lakini malipo ya muda wa kazi wa ziada kwa upande mwengine yamezidi mara mbili.

Polisi wanafahamika kuwa kundi la wafanyakazi ambalo wanaishi kwa fadhaa kupita kiasi. Vile vile, teknolojia ya polisi ambayo ilitakiwa iwe ya kisasa zaidi, imekuwa haiimarishwi inavyotakikana. Ni kweli kuwa polisi wenye sare zao hawawezi kumzuwia kila mshambuliaji wa kujitoa muhanga, lakini kila wakiwepo wengi kwenye maeneo ya umma, huwa panapatikana hisia za kuwepo kwa usalama.

Uimarishaji wa mashirika ya kijasusi

Hilo pia ndilo linaloyakabili mashirika ya kijasusi ya Ujerumani na nchi nyengine. Baada ya miongo saba ya amani na miaka 25 tangu kuanguka kwa ukomunisti, ni kituko kudhani kuwa tunaweza kuendelea nayo hivi yalivyo. Ni nani mwengine, kama si mashirika haya, ambaye angeweza kukusanya taarifa na kuzichambua kusudi kugundua na kuzima mashambulizi?

Mashambulizi mengi dhidi ya Ujerumani yamezuiwa huko nyuma, shukrani kwa taarifa za intelijesia za mashirika ya nje, lakini sio kwa ushahidi wa uwezo wetu wenyewe. Tunapaswa wenyewe kujielimisha juu ya harakati za makundi ya siasa kali za kidini ndani ya nchi yetu wenyewe.

Mwisho, ili kujuwa yanayoendelea, lazima kuyadhibiti mawasiliano ya mtandaoni, ingawa ulinzi wa faragha za mtu binafsi ni jambo takatifu kuweza kuguswa nchini Ujerumani. Lakini kwenye zama hizi za vitisho vya ugaidi, lazima tuweke vipaumbele. Ulinzi wa uhai wa binaadamu uwekwe kuwa wa muhimu zaidi kuliko ulinzi wa taarifa binafsi za mtu.

Mwandishi: Volker Wagener
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Bruce Amani