1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni kuhusu hatima ya siasa za Ujerumani

Ines Pohl | Oumilkheir Hamidou
29 Oktoba 2018

Sauti zinazidi kupazwa kudai SPD wajitoe katika serikali ya mseto inayoongozwa na Angela Merkel. Angela Merkel anaongoza serikali tangu miaka 13 iliyopita. Na umaarufu wake haujawahi hata mara moja kupungua kama sasa.

https://p.dw.com/p/37LRb
Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/S. Gollnow

Katika wakati ambapo mwishoni mwa wiki hii walimwengu walikuwa wakiomboleza kuuliwa wayahudi 11 mjini Pittsburg, nchini Ujerumani wafuasi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia "Chaguo Mbadala kwaajili ya Ujerumani" AfD wameingia katika bunge la mwisho ambako hawakuwa wakiwakilishwa.

Wamejikingia zaidi ya asilimia 12 ya kura katika uchaguzi wa bunge la Hessen-yanakokutikana makao makuu ya benki na taasisi za kiuchumi za Ujerumani, jimbo ambalo mishahara ni ya juu zaidi kuliko kwengine Ujerumani na pia idadi ya wasiokuwa na ajira inazidi kupungua tangu miaka kadhaa sasa.

Kinachotisha zaidi ni ile hali kwamba mmojawapo wa viongozi wa AfD aliyataja mauaji ya wayahudi yaliyofanywa na wanazi katika vita vikuu vya pili vya dunia, kuwa "uzushi wa historia". Na chama hicho hicho kinawakilishwa sio tu katika bunge la shirikisho Bundestag, bali katika mabunge ya majimbo yote 16 ya Ujerumani. Kimsingi hali hiyo ingebidi izushe mshutuko nchini na kuhanikiza magazetini kote nchini. Kwamba mambo hayako hivyo, ndio sababu kwanini AfD wanazidi kushuinda.

Sauti zinazidi kupazwa kudai SPD wajitoe katika serikali ya mseto inayoongozwa na Angela Merkel
Sauti zinazidi kupazwa kudai SPD wajitoe katika serikali ya mseto inayoongozwa na Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

 Angela Merkel anaongoza serikali tangu miaka 13 iliyopita. Na umaarufu wake haujawahi hata mara moja kupungua kama sasa. Aina fulani ya machofu pengine ndiyo chanzo cha hali hiyo. Na pia sera yake kuelekea wakimbizi imechangia. Na zaidi kuliko yote ni ile mivutano isiyokwisha serikalini. Serikali kuu ya vyama vya CDU, CSU na SPD ilikuwa tangu  mwanzo umoja wa lazima na sio wa mwelekeo ambao ungesaidia kuwaleta pamoja wananchi. Mashindano bayana na yasiyokwisha ya kuwania madaraka yamewachosha wapiga kura .

Idadi kubwa ya Wajerumani wamechoshwa na serikali hii ya mseto wa vyama vikubwa. Na hivyo hivyo ndivyo ambavyo uchaguzi katika jimbo loa Hessen umegeuka uchaguzi utakaoamua hatima ya Angela Merkel na serikali yake. Ingawa CDU wamepoteza kura kwa wingi lakini bado wao ndio  wenye wingi wa kura na hakuna serikali  ya mseto itakayoweza kuundwa mjini Wiesbaden bila ya wao. Hata mshiirika serikalini mjini Berlin,chama cha SPD kimeondolewa patupu-kimejikingia asili mia 20 na hizo katika jimbo ambalo kijadi ni gome ya wanasocial Democrat.

Baada ya zilizala hiyo ya kisiasa, sauti zinazidi kupazwa kudai SPD wajitoe katika serikali ya mseto inayoongozwa na Angela Merkel. Na mjadala huo unaonyesha utaendelea kwa namna ambayo utaizuwia serikali kuendelea na shughuli zake. Ni kishindo kikubwa na sio tu kwa Ujerumani bali pia kwa Ulaya.

Mwandishi:Ines Pohl/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman