1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma habebeki tena

28 Aprili 2016

Katika maadhimisho ya siku ya uhuru nchini Afrika Kusini chama cha ANC hakikuonyesha furaha. Katika maoni yake mkuu wa idara ya Afrika Claus Stäcker anasema hali hiyo inatokana na kashfa za Rais Jacob Zuma

https://p.dw.com/p/1Idcw
Malalamiko dhidi ya Rais Jacob Zuma bungeni
Malalamiko dhidi ya Rais Jacob Zuma bungeniPicha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Viongozi wa chama cha ANC bado wanajaribu kufanya mbinu za kuikabili hali iliyotokea .Bado wanajaribu kuzidhibiti athari za madhara yaliyosababishwa na Rais Zuma. Na bado wanaamini kuwa wataweza kupata suluhisho la ndani ili na hivyo kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa mnamo mwezi wa Agosti kwa mafaniko.

Lakini hakuna mwenye mashaka tena ndani ya chama cha ANC kwamba Zuma amekuwa mzigo usiobebeka. Ndani kwa ndani mapambano yanaendelea miongoni mwa wajanja, ya kugombania vyeo na viti vyao bungeni vinavyowahakikishia mishahara mizuri. Zuma amefanikiwa kujenga mtandao wa kifisadi ambao mpaka sasa umeweza kumlinda ili asianguke.

Chama cha Mandela kinajimaliza chenyewe

Watu wa nje wamepigwa na butaa kuona jinsi chama cha ANC, cha akina Luthuli,Tambo na Mandela kilivyoendelea kufarakana na malengo yake ya hapo awali. Watu wanashangaa kuona jinsi chama hicho kinavyojimaliza chenyewe haraka. Vyama vyingine vya ukombozi vilichukua muda wa miaka 50 kufikia hatua hiyo.

Baadhi ya wanachama waadilifu bado wanasisitiza juu ya moyo wa mshikamano wa hapo awali. Wanajaribu kuufufua kutokea ndani ya chama.Na kwenye mikutano ya faragha wanazungumza kinagaubaga! Wanalalamika juu ya utovu wa heshima na majikwezo ya viongozi wao walioivuruga imani yote ya chama cha ANC.

Watu hao wanasema ni kosa kuwaita watu wanaomkosoa Zuma kuwa wasaliti na wanalalamika kwamba viongozi wao wanayatelekeza maadili yanayokipa chama nguvu. Makada wa chama wanaomtupa mkono Zuma wazi wazi wanaongezeka waliopambana na utawala wa makaburu, waliofungwa jela pamoja na Mandela na mawaziri wa sasa.

Mkuu wa idara ya Afrika Claus Stäcker
Mkuu wa idara ya Afrika Claus StäckerPicha: DW

Na sasa kashfa ya Nkandla

Zuma alitumia mamilioni ya fedha za umma kukikarabati kijiji chake binafsi katika jimbo la Kwa -Zulu. Hukumu iliyotolewa na mahakama dhidi ya Zuma lilikuwa pigo kubwa. Zuma ameariwa kurudisha Euro Milioni 14.

Katika nchi nyingine Zuma angelilazimika kujiuzulu kwa hiari yake. Na hata sasa hiyo ingelikuwa njia bora kabisa ya kukiwezesha chama cha ANC kusonga mbele kama jumuiya ya umma. Hata hivyo njia bora zaidi ingelikuwa kumtimua Zuma.

Chama cha ANC kilikuwa na uwezo, wa kujibadilisha lakini sasa chama hicho tawala kimeipoteza nguvu hiyo. Kamati Kuu ya ANC imegawanyika juu ya suala la Zuma, lakini kwa bahati mbaya katika misingi ya ukabila .Tofauti kama hizo hazikuwapo hapo awali. Njia nyingine ni kusonga mbele kama hapo awali.Kutokana na kuwa na wabunge wengi, Zuma ana ngao thabiti bungeni, licha ya kukiuka katiba.

Pengo kati ya chama cha ANC na jamii nzima linazidi kupanuka na hivyo chama hicho kinazidi kutetereka kutoka kwenye misingi ya demokrasia.

Nkosazana Dlamini-Zuma

Njia nyingine inayowezekana ni kwa Zuma kung'atuka kimyakimya na kumwachia urithi Nkosazana Dlamini - Zuma aliewahi kuwa mkewe, anaemaliza muhula wake wa uenyekiti wa Umoja wa Afrika mnamo mwezi Julai. Mama huyo anayo sifa ya kuwa mchapa kazi na pia anakubalika katika pande zote za ANC. Tofauti na mwanasiasa mwengine, Cyril Ramaphosa anaeungwa mkono na matajiri.

Nkosazana Dlamini- Zuma atakabiliwa na jukumu la kuirejesha imani ya chama. Hizo zinaweza kuwa habari nzuri katika siku ya leo inayoadhimishwa kuwa ya uhuru nchini Afrika kusini.

Mwandishi:Claus Stäcker

Mfasiri:Mtullya Abdu.

Mhariri:Yusuf Saumu