1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Magufuli, rais aliyependwa kama alivyochukiwa

18 Machi 2021

Marehemu John Magufuli atakumbukwa kwa muda mrefu kwa pande zote mbili – uzuri na ubaya, anasema Mohammed Khelef kwenye ta'azia yake kwa kiongozi huyo wa Tanzania aliyetangazwa kufariki dunia hivi leo.

https://p.dw.com/p/3qmgQ
Tansania Präsident John Magufuli verstorben
Picha: AFP

Rais Magufuli anaondoka akiwa ana wengi wanaomkumbuka kwa dhati kabisa kama kiongozi mzuri na wa aina yake. Lakini pia anaondoka akiwa na wengi wanaoamini kuwa rais huyo aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 61 mjini Dar es Salaam alikuwa muovu wa kupindukia.

Khofu isiyoelezeka na mapenzi yasiyohojika ndilo eneo alilolitawala vyema zaidi kuliko alivyoweza kuitawala mipaka ya taifa hilo kubwa kabisa la Afrika Mashariki. Waliompenda walimpenda kikwelikweli na waliomchukia walimchukia kikwelikweli. Na wote walikuwa na sababu zao.

Kwa waliompenda, rais huyu aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2015 alikuwa mfano wa malaika aliyeletwa kwao kuliokowa taifa ambalo lilishatopea kwenye rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

Sifa hii ndiyo aliyotaka daima atajwe nayo na ndiyo aliyoipigia kampeni kuelekea Oktoba 2015. Ingawa ushindi wake haukuwa mkubwa sana panapohusika ushindi uliokuwa umezoeleka na chama chake, CCM, kinachoitawala Tanzania tangu uhuru hadi sasa, lakini ulimtosha sana kumkusanyia nguvu alizozitamani, naye akazitumia apendavyo.

DW Kiswahili | Mohammed Khelef
Mohammed Khelef wa Idhaa ya Kiswahili ya DWPicha: DW/L. Richardson

Tangu hapo, katiba ya Tanzania, kwa maneno ya wachambuzi wengi, inaunda taasisi ya urais ambayo haina tafauti sana na utawala wa kifalme.

Tanzania ya Magufuli

Magufuli aliitumia vyema taasisi hiyo ya urais kujenga Tanzania aliyoitaka mwenyewe. Neno "Tanzania ya Magufuli" lilikuwa la kawaida sana kutamkwa naye mwenyewe na wateule wake ndani ya serikali na chama chake, na kwa hakika walimaanisha hivyo.

Staili yake ya kutawala ilikuwa ni amri mkononi na mara kadhaa akijidhihirisha kama mtatuzi wa changamoto kubwa kubwa na ndogo ndogo kwa kasi ya papo kwa papo.

Lilikuwa jambo la kawaida sana kwake kufika sokoni, na kuamuru hapo hapo mkurugenzi wa manispaa aliyelalamikiwa na wafanyabiashara ndogo ndogo aondoshwe mara moja, au kutowa pesa kwenye begi yake na kumpa mwanamke aliyelalamika kuwa biashara yake ya maandazi imefilisika.

Siasa hizi za umashuhuri alizipenda na zilimpenda. Akaishi nazo ndani yake, nazo zikamfuata alipo. Ilifikia wakati wananchi walikuwa wanakusanya matatizo yao yote – makubwa, ya kiasi, na madogo – na kumsubiri yeye aje awatatulie. Ni kama kwamba hawakuwa wanamuamini msaidizi wake yeyote kuwa angeliwafanyia kile ambacho yeye angelikifanya.

Kutumbuatumbua, kuadhiri hadharani, kudhalilisha, na wakati mwengine hata kutisha, yalikuwa mambo yaliyowapendezesha wananchi wa kawaida, ambao waliamini yanafanywa kwa ajili yao.

Baina ya uchumagu na umagukrasia

Kwenye kiwango cha juu pia, Magufuli atatajwa na kuhusishwa na maamuzi makubwa ya ujenzi wa miundombinu kama vile mradi wa reli ya kati, bwawa la umeme la Stiglers‘ gorge, madaraja ya juu jijini Dar es Salaam, na pia umaliziaji wa miradi mikubwa iliyoanzia kwenye tawala zilizopita, na ambazo naye alikuwa sehemu yao akishikilia nafasi mbalimbali kwenye baraza la mawaziri la Benjamin Mkapa, rais wa awamu ya tatu, na Jakaya Kikwete wa awamu ya nne.

Kwa hivyo, masuala ya uwajibikaji serikalini na usimamizi wa sera za uchumi ambazo aliziamini kuwa ni sawa kwa wakati kwa Tanzania aliyoirithi kutoka kwa watangulizi wake, Magufuli alipendeza machoni mwa wale waliofaidika au ambao walioamini kufaidika na hatua zake. Mahala fulani niliuita uongozi wake kwenye eneo hili kuwa ni uchumagu - uchumi wa Magufuli.

Lakini, kuna upande mwengine wa Magufuli ambao haukuwapendeza – na kwa hakika hasa, uliwachukiza wengi. Huu niliuita na bado nauita magukrasia – mfumo wa utawala ambao unafuata matakwa ya Magufuli peke yake, hata kama matakwa hayo ni kinyume na katiba, sheria, kanuni, na utamaduni wa nchi na za kimataifa.

Rais wa kupiga marufuku

Kwenye hilo, Rais Magufuli alikuwa na mifano mingi mno kiasi cha kwamba kwa wengi hiyo ilikuwa ndiyo sura yake halisi.

Rais ambaye angeliamuru watoto wa kike waliopata ujauzito wasiruhusiwe kurejea masomoni baada ya kujifunguwa, hata kama hilo ni kinyume na katiba ya nchi na matamko ya kimataifa ambayo nchi imesaini.

Alikuwa rais ambaye angeliamuru vyama vya upinzani visifanye mikutano, mikusanyiko wala maandamano baada ya uchaguzi hadi msimu wa uchaguzi mwengine, kinyume kabisa na matakwa ya sheria ya nchi na utamaduni wa siasa za kidemokrasia.

Alikuwa rais ambaye angeliweza kupuuzia itifaki ya kimataifa kwenye vita dhidi ya janga la virusi vya corona na kuwataka wasaidizi wake wote wafuate utaratibu aliouweka yeye na ikawa hivyo.

Ndiye rais aliyefungia vyombo vya habari, kutishia waandishi, kuwakaba matajiri, wanaharakati na wanasiasa kwa kesi za uhujumu uchumi zisizokuwa na dhamana na wakasota ndani muda mrefu bila kesi zao kwenda popote.

Ndiye rais aliyesimamia nchi iliyopita chaguzi mbili – wa mabaraza ya miji, vijiji na miji mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, ambazo zote zinatajwa kuwa hazikuwa huru wala hazikuwa za haki.

Matokeo yake ni kuwa amekifanya chama chake cha Mapinduzi (CCM) kuwa mfano wa chama kimoja pekee cha kisiasa ndani ya Tanzania, kikiwa kinahodhi takribani asilimia 90 ya ofisi za umma.

Ndiye rais ambaye alijaribu kadiri ya alivyoweza kuifanya Tanzania isiwe sehemu ya ulimwengu uliyoizunguka, ikitafautiana takribani na majirani zake wote katika jambo moja ama jengine, iwe kibiashara au kisiasa.

Huyu ndiye Magufuli, ambaye kwa wengi ndiye sasa anayewaaga na kuiwacha nchi yake katika hali kama ilivyo – inayojaribu kujiinuwa kiuchumi, lakini iliyorudi nyuma sana kisiasa.

Kwa kila hali, alikuwa muumini wa siasa za hamasa zilizomfanya apendwe kwa kiwango kile kile alichochukiwa.