Maoni: Maswali mengi katika mkataba wa Minsk II
13 Februari 2015Ulikuwa mkutano mrefu wa usiku bila shaka na kwa kiasi fulani mkutano wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels ulichangia matokeo ya mkutano huu wa Minsk kuweza kufanikiwa. Kiongozi wa kwanza kuzungumza baada ya mkutano huo alikuwa rais Vladimir Putin wa Urusi, katika mkutano na waandishi habari , kwamba rais Poroshenko, kansela Merkel, rais Francois Hollande na yeye binafsi wamekubaliana kwamba pande zinazopigana zimeamua kusitisha mapigano mashariki mwa Ukraine kuanzia Februari 15.
Baadaye kansela wa Ujerumani akathibitisha hilo pamoja na rais wa Ufaransa Francois Hollande, ambapo walionesha matumaini ya tahadhari katika makubaliano hayo. Mtu anajiuliza hata hivyo, matumaini haya yanaelekeza wapi. Kumalizika kwa mapigano na mauaji mashariki mwa Ukraine bila shaka ni jambo la kufurahisha. Lakini kwa mtazamo wa hali ilivyo kwa hivi sasa , ni kwamba makubaliano hayo yanaleta shaka zaidi kuliko kile kinachotarajiwa.
Wadadisi wanasema kwamba vipengee vya makubaliano haya, ya mkataba mpya wa Minsk, haviendi mbali zaidi ya makubaliano ya mkataba wa kwanza wa Minsk, ambao ulitiwa saini mapema mwezi wa Septemba mwaka jana. Katika mkataba huo pia kulikuwa na makubaliano ya kusitisha mapigano na kuondolewa kwa silaha nzito, lakini makubaliano haya hayakuheshimiwa.
Je mapigano yatakoma?
Wakati huo huo wapiganaji ambao wanapewa msaada na Urusi wameweza kukamata maeneo muhimu katika operesheni zao. Muhimu katika mapambano hayo ni eneo muhimu la usafiri wa treni katika mji wa Debalzewe, ambao wapiganaji wanaotaka kujitenga wameuzingira, lakini majeshi ya Ukraine yanapambana kuulinda mji huo.
Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano yanaanza rasmi katika siku mbili zijazo, si rahisi kwa hiyo kuondoa uwezekano, kwamba wapiganaji watataka kuukamata mji huo muhimu na mapambano kuzidi, ili kuweza kuwa na karata muhimu katika makubaliano hayo.
Inabakia hata hivyo wasi wasi mkubwa kutokana na misingi mingine, iwapo makubaliano hayo yatakayoanza Februari 15 yataheshimiwa. Makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yanaweza kufanikiwa, iwapo eneo litakaloundwa la kutokuwa na shughuli za kijeshi litawekewa uangalizi wa kutosha na kuheshimiwa.
Haifahamiki iwapo shirika la usalama na ushirikiano barani Ulaya OSCE litaweza kutumika, kwasababu katika mkataba huu mpya kuna maneno ya juu juu tu kuhusu kazi za uangalizi. Kwa hiyo inawezekana kabisa kwamba mapambano yakaendelea.
Mwandishi: Mannteufel , Ingo / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Iddi Ssessanga