Maoni: Matumaini yatokanayo na diplomasia kuhusu Libya
20 Januari 2020Kwa muda mrefu Ujerumani imekuwa ikihangaika kutaka kuchukua nafasi ya kuwajibika kimataifa. Mara nyingi haiko wazi, iwapo hilo si suala linalobishaniwa. Je uwezo wa kijeshi ni mbaya. Nafasi za Ujerumani na urithi wa historia yake inaifanya iwe katika nafasi finyu sana. Lakini bila shaka, nguvu za Ujerumani zinaweza kusaidia kwa kuitazama hapo zamani pamoja na uwezo wake wa kidiplomasia.
Jana Jumapili Kansela Angela Merkel alikutana mjini Berlin na marais wa Ufaransa, Urusi , Uturuki na Misri. Pia mawaziri wakuu wa Uingereza na Italia. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, pamoja na wawakilishi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika. Libya ambayo inapitia katika mzozo mkubwa, iliwakilishwa na pande zote zinazohusika katika mzozo huo. Kiongozi wa serikali inayotambulika kimataifa Faiz al-Farraj na mbabe wa kivita jenerali Khalifa Haftar ambaye anadhibiti sehemu kubwa ya ardhi ya nchi hiyo.
Lakini tukio la kuwapo katika mkutano huo viongozi wote wanaohusika katika mzozo huo, bila ya wao kukutana ana kwa ana lina maana kubwa kuhusiana na hali ya mzozo nchini Libya. Tangu pale alipoangushwa kutoka madarakani kiongozi wa muda mrefu wa Libya, Mouammar Gaddafi, mwaka 2011, nchi hiyo inajikuta katika vita vinavyoendelea, ambamo mataifa kadhaa ya nje yanahusika.
Hapa kuna masuala ya mafuta na gesi na wakimbizi, ambao wahalifu kutoka nchini Libya wanasaidia kuwasafirisha kupitia bahari ya Mediterania, ama kuwashikilia nchini Libya katika hali mbaya kabisa.
Na pia kuna suala la ugaidi wa makundi ya Kiislamu. Mchanganyiko wa vurumai lote hilo kwa muda mrefu haukuwa ukiangaliwa kama ilivyokuwa katika vita nchini Syria. Lakini vita vya mataifa mengine vinavyopiganwa nchini Libya, ni mzozo wa muda mrefu.
Serikali ya Ujerumani ilianzisha juhudi za kupambana na hali hiyo, na kuyaita mataifa yenye ushawishi na nguvu katika mkutano wa Berlin, kuweza kuzungumzia kwa uwazi, pamoja na utendaji, kuweza kuwaleta pamoja viongozi wanaopambana nchini Libya kwa ajili ya upatanishi, hususan kuzuwia mtandao wa kimataifa unaounga mkono vita, upelekaji wa silaha na kujinufaisha kiuchumi.
Bila ya usaidizi wa kimataifa, kila kitu kingesimama, si upande wa serikali inayoungwa mkono kimataifa ama mbabe wa kivita Haftar, kusingewezekana kuchukua hatua.
Kwa Ujerumani kujiingiza katika hatua za kidiplomasia ilikuwa sahihi. Katika nyakati hizi za siasa kali za kizalendo, mpango huo binafsi unatambulika na Umoja wa Mataifa kuwa ni suluhisho halisi la Libya. Sasa hatua ya kusitisha mapigano na jumuiya ya kimataifa kuangalia usitishaji huo vinaweza kupatikana pamoja na utimizaji wa masharti ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.