1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

COP27 - Afrika iko peke yake

DW Kiswahili | Tatu Karema
Tatu Karema
22 Novemba 2022

Mataifa ya Kaskazini mwa dunia yameondoka mkutano wa mabadiliko ya tabianchi bila makubaliano ya maana kwa Afrika. Ni ukumbusho wa kusikitisha kwamba bara hilo liko peke yake katika suala la mabadiliko ya tabianchi.

https://p.dw.com/p/4JpMm
Kenya I Turkana region ravaged by prolonged drought
Picha: DW

Baada ya mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi ya COP27 mjini Sharm el-Sheikh, viongozi wa Afrika lazima waanze mara moja kupanga upya mikakati yao.

Sasa, zaidi ya hapo awali, bara la Afrika linahitaji kufikiria jinsi mamilioni ya watu walio katika hatari ya kukabiliwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi wanavyoweza kusaidiwa.

Ukweli wa mambo ni kwamba ufadhili kutoka kwa mataifa tajiri kusaidia kupunguza athari za ongezeko la joto duniani sio chanzo cha kutegemewa tena.

Idadi ya wanaokabiliwa na njaa inatarajiwa kuongezeka

Njaa inayotokana na ukame inatabiriwa kufikia kiwango cha hatari katika eneo la Pembe ya Afrika.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa kutokana na hali hiyo, mamilioni ya Waafrika walio katika mazingira magumu wanajiandaa kukabiliana na njaa kali katika kipindi cha miezi ijayo.

Mtazamo huu mbaya hauwezi kusubiri mazungumzo yasiyo na mwisho ya mabadiliko ya tabianchi.

Bara la Afrika lazima likubali kuwa liko peke yake na lichukuwe hatua za haraka kusaidia watu wake wanaokabiliwa na njaa ya mara kwa mara.

Hali ya kutoaminiana yaongezeka

Ingawa ni muhimu, mazungumzo juu ya mabadiliko ya tabinachi yamesababisha tu kuongezeka kwa hali ya kutoaminiana kati ya mataifa ya Kusini na Kaskazini mwa dunia.

Haya yanatokea wakati mamilioni ya Waafrika wanaendelea kuathirika kila siku na joto kali ambalo limechochewa na uchimbaji na matumizi ya mafuta ya visukuku, unaofanywa hasa na mataifa tajiri, ambayo ndio wachafuzi wakuu.

Wale wanaoteseka wanangoja kwa subira hatua kabambe za kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kufikiwa kupitia mazungumzo.

Wakati wa kuchukua hatua ni sasa, na viongozi wa Kiafrika hawawezi kudai kuwa wameishiwa na mawazo ya kuokoa watu wanaoteseka.

Hasa kuna wazo la kubadilisha hali hiyo ambayo viongozi wamekuwa wakilirejesha nyuma kwa miaka 20 sasa.

Kuongeza matumizi katika kilimo

Kenia Landwirtschaft
Wakulima watayarisha shamba kwa upanzi katika kaunti ya Kericho, KenyaPicha: Billy Mutai/Sopa/Zuma/picture alliance

Mwaka 2003, serikali za Afrika zilijitolea kutumia asilimia 10 ya bajeti yao ya kila mwaka katika maendeleo ya sekta ya chakula na kilimo.

Ahadi hii kubwa ilijulikana kama Tamko la Maputo. Nia yake ilikuwa ya ukakamavu, inayoweza kufikiwa na yenye maana. Wazo lilikuwa kupunguza uhaba wa chakula wa mara kwa mara kwa watu walio hatarini zaidi barani Afrika ifikapo mwaka 2030.

Kufikia sasa, nchi kadhaa za Kiafrika bado zinajikokota kutekeleza wazo hili. Nchi nyingi bado zimeweka mgao wao wa kila mwaka kwa sekta ya kilimo katika asilimia 4, miongoni mwao zikiwa ni Kenya, Uganda na Senegal.

Hofu ya mabadiliko ya tabianchi inalikumbusha bara hili kwamba utekelezaji wa Tamko la Maputo unahitajika sasa kuliko hapo awali.

Na huku pesa za wachafuzi wa mazingira matajiri zikiwa zimekwama mifukoni mwao, Afrika inapaswa kuzingatia kilimo kama suala la kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

Kilimo, uwezo mkubwa wa bara Afrika usiotumika

Jukumu kuu la sekta ya kilimo kwa bara la Afrika si la kutiliwa chumvi. Ndiyo tegemeo la mamilioni ya watu katika masuala ya kazi na mapato.

Kwa sasa, licha ya vikwazo vingi na kukandamizwa kwa mgao wa rasilimali, sekta hiyo bado ni chanzo cha mapato kinachotegemewa.

Viongozi wengi wamesisitiza dhamira ya serikali zao za kufufua sekta hiyo lakini yote haya yamegeuka kuwa maneno matupu.

Kwanini kupuuzwa basi?

Baadhi ya wachumi wanahoji kuwa muktadha wa sasa wa fedha wa bara hilo unafanya kuwa vigumu kwa sekta ya kilimo kuchangia asilimia 10 ya bajeti yote.

Hii ni kwa sababu tawala nyingi za Kiafrika zina mzigo mkubwa wa madeni ambao yanatumia bajeti zao kwa kiasi kikubwa.

Baadhi ya mataifa pia yametoa kipaumbele katika sekta nyingine muhimu, kama vile usalama, utalii, miundombinu na elimu

Lakini kwa kuzingatia nyakati ngumu zinazokuja, ambazo kwa kiasi fulani zimesababishwa na mabadiliko ya tabianchi, je, ni jambo kubwa kuuliza kwamba ugawaji upya wa bajeti ya matumizi uelekezwe kwenye sekta ya kilimo?

Matumizi ya juu kwa kila mtu yanahusishwa na utendaji kazi bora wa sekta ya kilimo na, kwa hivyo, ni hatua ya tahadhari inayostahili kuchukuliwa.

Iwapo yote yatafanyika kwa njia ipasayo, sekta ya kilimo inaweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato na hata ikaweza kufadhili sekta nyingine.

Zaidi ya hayo, ongezeko la joto duniani limefanya iwe muhimu zaidi kuongeza utafiti katika eneo hilo, ambao pia utalazimika kufadhiliwa ipasavyo.

Bara la Afrika linahitaji kuendeleza na kutumia aina za mazao yanayostahimili hali tofauti za hewa, maghala yanayoweza kudhibiti wadudu na teknolojia za hali ya juu.

Msukumo huu wa mabadiliko unaweza kutekelezwa kwa ushirikiano na mazungumzo ya haki ya mabadiliko ya tabianchi. Na matokeo yake yanatarajiwa kuwa ushindi kwa bara zima.