Maoni: Mchezo umekwisha, EU na Uingereza
24 Juni 2016Mwandishi wa DW Rob Mugde anaandika katika uhariri wake kwamba mchezo umekwisha na umoja huo wenye makao yake makuu mjini Brussels, unatakiwa kujilaumu wenyewe.
Katika kitabu chake kwa jina "Pride and Prejudice", yaani "Fahari na Chuki" mwandishi wa vitabu Jane Austen, alitumia sentensi muhimu kuelezea hisia za mtu aliyekuwa katika mapenzi jinsi alivyochoshwa na uhusiano wake: "Watu wenye hasira hawana busara wakati wote."
Maneno haya yakitumiwa katika uamuzi wa Uingereza, yana maana watu wengi wenye hasira wameilazimisha Uingereza kujiondoa kutoka kwa Umoja wa Ulaya. Kutakuwa na hasira na hali ya kukata tamaa jijini London na katika miji mikuu ya nchi za barani Ulaya.
Na ni haki kabisa. Kuna mambo mengi ya kukasirisha. Hasira dhidi ya waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kwa kuruhusu kutekwa nyara na wanachama wa chama chake wasiopendelea Umoja wa Ulaya na kumlazimisha aandae kura ya maoni. Sasa tunafahamu vipi suala hili lilivyokuwa mchezo mkubwa wa kamari na tathmini isiyo sahihi kwa nchi nzima na kwa yeye mwenyewe binafsi.
Ghadhabu pia dhidi ya kauli kali za kizalendo, tetesi za kutia hofu zilizotolewa na waliounga mkono Uingereza ijitoe Umoja wa Ulaya, zilizopokewa vizuri zaidi na kukubalika zaidi kuliko hoja za wale waliotaka nchi hiyo ibakie katika umoja huo.
Hasira pia kwa makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels kwa kujiridhisha kwamba kila kitu kilikuwa shwari na jinsi ulivyoenea na kujiingiza katika taasisi za Ulaya kama ugonjwa wa mlipuko katika miongo kadhaa iliyopita, huku ukishindwa kutilia maanani masilahi na matakwa ya mataifa kama vile Uingereza.
Kama waandaaji wa mkataba wa Maastricht na mageuzi ya mkataba huo, na Mkataba wa Lisabon wangezingatia kuwa na muungano kamili wa kisiasa badala ya kuzingatia tu muungano wa kiuchumi, pengine hatungekuwa katika hali ngumu inayotukabili leo - mgogoro wa kiuchumi wa Ugiriki, mzozo wa wakimbizi na sasa kujitoa kwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya.
Si uamuzi wa kushangaza
Lakini tuchukue hatua moja nyuma na tujiulize. Je tumeshangazwa? Je Uingereza haijakuwa wakati wote nje zaidi kuliko ndani ya Umoja wa Ulaya? Waingereza wamekuwa mara zote wakinufaika na hali yao ya kuwa kama kisiwa nje ya umoja huo wakikaa kando kando, wakichukua majukumu madogo na kutizama mambo yanavyokwenda Ulaya.
Kura ya maoni ingekuwa fursa muhimu sana kwa Uingereza kupiga kura kubakia katika Umoja wa Ulaya ili kuwa sehemu ya soko la uchumi wa kijamii ililosaidia kuliunda, na kuweza kufuatilia kile ambacho waziri mkuu David Cameron, alifanikiwa kupata mageuzi hatua kwa hatua mjini Brussels katika miezi ya kuelekea kura ya maoni.
Je Uingereza itasambaratika? Scotland imesema ina haki ya kufanya kura ya pili ya maoni kujitenga na Uingereza na kujiunga na Umoja wa Ulaya. Ireland Kaskazini huenda ikafuata mkondo huo. Je England inaweza kuamua kujitoa kutoka kwa muungano wa Uingereza? Meya wa jiji la London, Sadiq Khan anaweza kuhoji kwamba London haikupiga kura kuunga mkono Uingereza itoke Umoja wa Ulaya na sasa anaichukulia serikali kwamba haifanyi kazi, ingawa swali la kuuliza ni je imewahi kufanya kazi?
Kwa Ujerumani matokeo ya kura ya maoni ni kama ndoto mbaya. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na waziri mkuu Cameron wangeunda ushirikiano ambao ungesaidia sana kuleta mageuzi yanayohitajika mjini Brussels. Bila shaka kuna wale watakaohoji kwamba Wajerumani sasa hawataweza tena kutoa amri kwa Waingereza, lakini litakuwa jambo la kusisimua kuona ni vipi biashara za Uingereza zitakavyofanikiwa kupiga hatua bila teknolojia na mchango wa Mjerumani.
Mwandishi: Rob Mudge/DW
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri:Saumu Yusuf