Maoni: Merkel na Putin - Si marafiki lakini ni washirika
13 Januari 2020Katika uhariri ulioandikwa na mwandishi wa DW Juri Rescheto, anajiuliza iwapo Urusi na Umoja wa Ulaya sasa zinaelekea kukaribiana zaidi. Hili mhariri anaandika kuwa lingekuwa jambo zuri kutokana na hali ilivyo katika mashariki ya kati.
Nchini Urusi kuna msemo usemao, "Niambie, nani ni adui yako , na nitakwambia wewe ni nani." Angela Merkel na Vladimir Putin si marafiki kabisa, lakini ni washirika, katika uchumi na siasa. Pamoja na vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi pamoja na mauaji ya raia wa Urusi mjini Berlin, pamoja na kuliingiza katika himaya yake eneo la Crimea na vita katika eneo la Donbass nchini Ukraine, pamoja na tofauti za kisiasa , viongozi hao wanakaribiana kuliko viongozi wengine. Merkel anamhitaji Putin. Ulaya inaihitaji Urusi.
Iwapo mtu anapenda ama la, ukweli ni kwamba ushawishi wa Urusi katika mashariki ya kati ni mkubwa. Hususan kutokana na hali ya kuwa na ombwe la uongozi, ambalo Marekani imeliacha, Urusi imesongambele katika hilo katika eneo lote.
Nchini Libya, ambako kuna hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kupamba moto na ambako kunaweza kutarajiwa mmiminiko mwingine wa wakimbizi kuelekea Ulaya.
Nchini Syria , ambako Putin amesema kuwa yuko upande wa kiongozi wa nchi hiyo Bashar al-Assad kijeshi. Nchini Iran , rais huyo wa Urusi anajionesha wazi kuwa ni mshirika.
Putin anaweza kutumika katika utatuaji wa mizozo yote hii. Na hilo analifahamu. Na anaamini kuwa ni mtu muhimu , kama anavyoonekana katika medani ya kimataifa, kwamba haiwezekani kumuachia yote haya peke yake, kwamba Urusi nchini Syria sio mchochezi wa vita , badala yake anachukuliwa kama ni mpatanishi wa amani. Na hatimaye vikwazo vya mataifa ya magharibi vinaweza kulegezwa siku za baadaye.
Swali baada ya mazungumzo ya masaa mawili mjini Moscow ni iwapo Ujerumani iko tayari, kuingia katika ushirikiano mpya, ambao utaiweka nchi hiyo mbali na Marekani. Tangu pale Donald Trump kuwaona Merkel na Putin kuwa ni maadui, katika masuala ya uchumi na siasa, Ujerumani inahitaji kwa udi na uvumba gesi kutoka Urusi kupitia mradi mkubwa wa bomba la Nord Stream 2, Marekani inataka kuzuwia mradi huo kwa njia yoyote ile. Ndio sababu mawaziri wa mambo ya kigeni wa Urusi na Ujerumani wamezungumzia tofauti kuhusu kuuwawa kwa jenerali wa Iran Qassem Soleimani na Marekani.