1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Mkutano wa kilele kati ya Ulaya na China wakosa tija

15 Septemba 2020

Mkutano wa kilele kati ya Ulaya na China wa mwaka huu ulitarajiwa kuwa nuru ya mafanikio ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, lakini badala yake umeambulia patupu. Pengine, COVID-19 imemwepusha aibu kansela huyo.

https://p.dw.com/p/3iTVo
EU-China-Gipfel zu Markenschutz
Picha: Reuters/Y. Herman

Awali mkutano huo kati ya Umoja wa Ulaya na China ulipangwa kufanyika mwezi Juni katika mji wa Leipzig mashariki mwa Ujerumani kwa siku tatu, na kwa mara ya kwanza rais wa China Xi Jinping angepata fursa ya kukutana ana kwa ana na viongozi wa nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya. Janga la corona limeuhamishia mtandaoni mkutano huo, na kuufupisha kuwa wa siku moja. Hata hivyo, mafanikio yake yamekuwa madogo, madogo mno.

Mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na China kwa wakati huu yamedorora katika kiwango kibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa. Pande hizo zinatofautiana juu ya mienendo ya China kisiwani Hong Kong, ukiukaji wa haki za binadamu katika jimbo la Xinjiang, ubabe wa China katika Bahari ya China Kusini, na vitisho vya Beijing kwa Taiwan.

Tofauti za kimaadili zakorofisha mambo

Bernd Riegert, Korrespondent, Studio Brüssel
Bernd Riegert, Mwandishi wa DW

Viongozi wa Umoja wa Ulaya, Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel, Rais wa Halmahauri ya Ulaya Ursula von der Leyen na Kansela wa Ujerumani na mwenyekiti wa baraza la Ulaya Angela Merkel, wameyataja matatizo hayo bayana, lakini Rais Xi Jinping wa China haelewi chochote katika lugha ya uhuru wa kujieleza na haki za binadamu, na hakuashiria kuzingatia malalamiko ya Ulaya.

Charles Michel aliikumbusha China kuwa uhusiano kati ya China na Ulaya unapaswa kuwa katika misingi ya usawa, kwa sababu Ulaya sio uwanja wa China kuchezea, bali pia ni mchezaji katika uwanja wa kidunia. Lakini China ni taifa la utawala wa kiimla wa chama kimoja, na kuihubiria maadili ya kimagharibi, ni kama kutwanga maji kwenye kinu.

Ni vigumu kwa mfumo wa kisiasa wa Ulaya na ule wa China kutangamana, kwa sababu ni ya ushindani.

Kupigania maslahi bila kunyoosha mikono

Umuhimu wa China unatokana na kasi ya maendeleo yake kiuchumi, na Kansela Angela Merkel anasema China imeiamarika vya kutosha kutazamwa kama mshindani. Ulaya, na hasa Ujerumani inaihitaji China katika juhudi za kuukwamua uchumi wake ulioathiriwa na janga la corona, lakini China pia inaihitaji Ulaya.

Ulaya imefanikiwa kuzungumza kwa sauti moja katika mkutano wa vidio jana Jumatatu, katika kudai haki sawa kwenye soko la China na usalama wa mitaji inayowekezwa nchini humo. Madai hayo ya Ulaya yanaendelea kupuuzwa na Beijing, na ni kutokana na hali hiyo kwamba makubaliano ya uwekezaji yaliyotarajiwa kusainiwa katika mkutano huu, hayakuwezekana.

Mwisho wa yote, mkutano kati ya Umoja wa Ulaya na rais wa China anayetajwa kuwa 'mtu aliyejipambanua', haukuwa wenye tija. Lakini, inavyoelekea, kila upande utaendelea kusimamia maslahi yake bila kusalimu amri kwa mwingine.

 

Bernd Riegert