Maoni: Pigo kwa haki za binadamu
24 Februari 2014Sheria hii ni pigo kubwa kwa haki za binadamu Uganda. Isitoshe, sheria hii ni ishara ya hatari kwa marais wengine wa nchi za Kiafrika. Mashirika ya kutetea haki za binadamu pamoja na wanasiasa wa nchi za Magharibi walimwekea shinikizo rais Museveni ili asitie saini muswada huo. Wiki iliyopita, rais Barack Obama wa Marekani alimtishia Museveni kwamba ataiwekea Uganda vikwazo vya kiuchumi iwapo atasaini muswada huo. Lakini inaelekea kwamba shinikizo kutoka nje halikuwa kubwa kama shinikizo alilowekewa Museveni na raia wake wenyewe.
Yoweri Museveni, ambaye sasa ana umri wa miaka 69 na ambaye amekuwa rais kwa miaka 28 sasa, anataka kuwa kama rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na kubakia madarakani hadi afikishe miaka 90. Uchaguzi ujao utafanyika Uganda mwaka 2016. Kwahiyo Museveni anaitumia nafasi hii kujipatia kura za raia wengi walio na mtazamo wa kihafidhina.
Ndugu pia hatarini
Katika nchi nyingi za Kiafrika ushoga ni jambo ambalo kamwe halizungumziwi. Maoni ya wengi ni kwamba ushoga ni ugonjwa. Hata kamisheni yenye wataalamu na madaktari ambayo hivi karibuni ilitoa ripoti iliyolenga kuthibitisha kwamba ushoga si ugonjwa, haikutosha kubadilisha mawazo ya Museveni. Ripoti hiyo haikumgusa Museveni hata kidogo, badala yake alisema kuwa ripoti haikuonyesha chanzo cha ushoga ni nini hasa. Hofu na uadui dhidi ya mashoga nchini Uganda inachochewa pia na ushawishi mkubwa wa makanisa ya kipentekoste na wahafidhina wa kundi la Teaparty kutoka Marekani.
Sheria iliyopitishwa jana si kwamba inafanya mashoga na wasagaji waweze kufungwa kifungo cha maisha tu bali hata wale wanaowazunguka wako hatarini kufikishwa mbele ya sheria. Ndugu zao, madaktari wanaozungumza nao, au hata mashirika ya kutetea haki za mashoga yanaweza kuadhibiwa. Hii ni kwa sababu sheria mpya inawataka raia wa Uganda kuwaripoti watu wote wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Marais wataka kufunga raia macho
Jambo la kusikitisha ni kwamba sheria hii imepitishwa Uganda, nchi ambayo ilikuwa mfano bora katika kuelimisha watu juu ya ukimwi. Je, ni nani ambaye sasa atathubutu kwenda katika kituo cha ushauri nasaha wakati anahofia kuwa anaweza kushtakiwa au hata kupelekwa jela?
Katika katiba ya Uganda kipo kifungu kinachotetea utu wa binadamu. Haki za binadamu ni sawa kwa watu wote, bila kujalisha wanaishi nchi gani. Kila mtu ana haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, dhidi kupigwa au kushtakiwa bila kosa, bila kujali anashiriki mapenzi ya aina gani. Ni ishara ya kusikitisha na ya kutisha kuona kwamba marais wa Kiafrika wanaong'ang'ania madaraka wanataka kuwanyima raia wao haki hizo au kuwafunga raia macho ili wasifuatilie matatizo mengine yaliyopo nchini kama vile alivyofanya rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye pia amepitisha sheria kama hii ya Uganda.
Mwandishi: Andrea Schmidt
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Saumu Yusuf