Maoni: Siku ya wanawake duniani wanawake wanapaswa kujiamini
9 Machi 2020Lakini, nje ya mfumo wa siasa za kibunge inaonekana wanawake wanapata nguvu zaidi, kama anavyoeleza Anja Brockmann katika uhariri wake kuhusu siku ya kimataifa ya wanawake, hapo jana.
Ukiangalia hali ya maendeleo ya wanawake duniani , unaweza kuingiwa na mashaka kidogo. Nchini Marekani mwaka huu pia hakutakuwa na mwanamke katika uongozi wa juu kabisa nchini humo. Nchini Afghanistan wanawake wanakabiliwa na kitisho cha kurudi nyuma katika enzi za giza kutokana na mkataba uliotiwa saini baina ya Marekani na kundi la Taliban. Na katika bara la Ulaya mpango wa rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen , kutaka halmashauri yake iwe na usawa wa wanawake na wanaume unapata upinzani kutoka kwa viongozi wa nchi wanaume.
Wanawake kupata uongozi wa kisiasa duniani kote bado linabakia kuwa suala la nadra sana. Ni nadra sana, ambapo ikitokea basi vyombo vya habari huiona ni habari kubwa sana, kama ilivyotokea hivi karibuni kwa waziri mkuu wa Finland Sanna Marin, ambaye sio tu mwanamke, lakini pia ni kijana na kwa hiyo ni hali ambayo si ya kawaida mara mbili. Katika mabunge mengi humu duniani , wabunge wanawake wamo katika kifungu cha idadi ya wachache, licha ya kuwa wazo la kuwa na demokrasia ya bunge kama kioo cha jamii inapingana nayo.
Na bila shaka , hata mwanamke mwenye madaraka makubwa duniani, Angela Merkel , katika nchi yake Ujerumani ameshindwa kupata nguvu ya kusema na kuwasaidia wanawake katika chama chake kuweka mfumo wa kuwa na kiwango fulani cha wanawake ili kuwa na ushawishi wa kutosha. Kwa hiyo si ajabu, kwamba kwa hivi sasa mwanachama mwezake katika chama chake Friedrich Merz, ambaye angependa sana kuwa kansela wa Ujerumani, amelalamikia kuhusu ubaguzi dhidi ya wanaume, akinyooshea kidole orodha ya wagombea wa kiti cha mwenyekiti wa chama, kwamba kuna wanawake wengi kuliko wanaume.
Na kutokana na hali hiyo, orodha ilibadilishwa. Hata hivyo kuna wanawake , ambao hawajiweki nje ya siasa. Wale ambao hakuna mwanamume ambaye anaweza kuwapita. Wanawake kama Greta Thunberg , ambaye kitisho cha maafa ya mabadiliko ya tabia nchi ameyaweka katika ajenda ya kisiasa duniani. Wanawake kama Carola Rackete, ambae kutokana na kazi yake ya uokozi kwa wahamiaji wanaosafiri baharini amepambana na waziri wa mambo ya ndani wa Italia. Wanawake kama Emma Gonzalez , ambaye anapambana kuimarisha sheria ya umiliki wa silaha nchini Marekani.
Mashujaa hawa wapya wa kisiasa ni vijana, wenye hasira na wanasukuma mambo fulani, katika upinzani nje ya mabunge. Ni nguvu mbadala dhidi ya wanaume kama Donald Trump, Vladimir Putin na Jair Bolsonaro. Wanataka kuamsha hali fulani, bila wao kuwa na madaraka. Na wanajiweka katika hatari, hatari ya kuchukiwa na wanaume. Hata hivyo thamani ya majina yao ina leta matumaini ya mwelekeo mpya wa kisiasa. Wanakuwa kioo cha wanawake vijana duniani kote.