1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Siku ya Wanawake haina mengi ya kuadhimisha Afrika

8 Machi 2021

Machi 8 ni siku ya wanawake duniani - siku ya kusheherekea mafanikio na mchango wa wanawake. Lakini wakati wanawake zaidi wanaendelea kuteseka, hakuna mengi ya kusherehekea Afrika, anaandika mwandishi wa DW Mimi Mefo.

https://p.dw.com/p/3qMae
Südafrika Johannesburg Demonstration Vergewaltigung
Picha: picture-alliance/dpa

Siku ya Wanawake duniani inafaa kusheherekea matunda ya miongo kadhaa ya uanaharakati. Hata hivyo, barani Afrika mambo ni tofauti kwani watuhumiwa wa makosa ya unyanyasaji wa kijinsia aghalabu hukwepa mkono wa sheria, kwa hio ni kipi cha kujivunia?

Kauli mbiu ya mwaka huu 2021 ni "Wanawake katika Uongozi: Kufikia fursa sawa siku za usoni katika uliwengu wa Covid-19". Licha ya kauli mbiu hiyo, mtu anapata wakati mgumu kuikumbatia hasa ukizingatia maumivu na uharibifu uliosababishwa na janga la Covid-19 haswa kwa wanawake.

Hakika kumekuwa na mwanamke bomba, kwa mfano aliyevumbua chanjo ya Pfizer BioNTech dhidi ya ugonjwa wa Covid-19. Bila shaka hatua hiyo inafaa kupigiwa mfano.

Lakini je, vipi kuhusu wanawake ambao wamepoteza dira yao ya maisha katika kipindi cha miezi 12 iliyopita?

Kwa bahati mbaya, siku ya wanawake duniani inaendelea kupoteza umuhimu wake. Kwa mfano nchini Cameroon, asilimia 43.2 ya wanawake nchini humo, wengi wanakabiliwa na visa vya unyanyasaji na hata kupigwa wakiwa majumbani karibu kila siku.

Kutokana na madhila wanayopitia wanawake, je kuna sababu ya kusheherekea siku hii?

Si hayo tu, ni hivi majuzi ambapo Makamu wa Rais wa Zimbabwe Kembo Mohadi alipojiuzulu kufuatia kashfa za ngono. Ni nadra sana kwa mwanasiasa wa Kiafrika kujiuzulu kutokana na kashfa za ngono na Makamu huyo wa Rais bila shaka ameweka rekodi mpya barani Afrika.

Kamerun Journalistin Mimi Mefo
Mwandishi wa DW Mimi Mefo.Picha: Mimi Mefo

Vile vile, nani anaeweza kusahau kisa cha Fezekile Ntsukela Kuzwayo ambaye alimtuhumu rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma kwa ubakaji, madai yake yakizua mjadala wa kitaifa nchini humo. Kwa mujibu wa kundi la kutetea maslahi ya wanawake nchini humo "Rape Crisis" ni kuwa asilimia 40 ya wanawake nchini Afrika Kusini hukabiliwa na ubakaji angalau mara moja katika maisha yao.

Wakati kesi hiyo ilipofikishwa kortini mwaka 2005, wakati huo Zuma alikuwa kiongozi wa chama cha ANC. Lakini licha ya ushahidi mzito dhidi ya Zuma, iliamuliwa kuwa wawili hao waliridhia kufanya mapenzi. Mwaka mmoja baadaye, Zuma alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo, wadhifa alioushikilia kwa karibu muongo mmoja.

Katika muhula wake wa uongozi, Zuma aliwatolea wito watu kuoga baada ya kufanya ngono ili kukabiliana na virusi vya HIV, na pia kutoa kauli kuwa sio kawaida kwa wanawake kukaa bila kuolewa miongoni mwa kauli nyengine tata.

Ndoa za utotoni pia zimeipaka tope Afrika. Mfano hai ni kisa cha seneta wa Nigeria Ahmad Sani Yerima ambaye alimuoa msichana mwenye umri wa miaka 13 kama mke wake wa nne mnamo mwaka 2010. Wakati huo, seneta huyo alikuwa na umri wa miaka 49 huku akitetea ndoa hiyo akisema dini yake inamruhusu.

Vikwazo na maneno makali pekee havitoshi kukabiliana na ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia. Kunahitajika juhudi za pamoja kote ulimwenguni. Hata hivyo, la kushangaza ni kuwepo kwa ukimya hasa kutoka kwa wanasiasa ambao wanaonekana kulemewa na tatizo la wasichana kutekwa nyara mara kwa mara nchini Nigeria.

Haijajulikana wazi ni kitu gani hasa wanachopitia wasichana hao wanapochukuliwa mateka, lakini mtu anafaa kujiuliza kwa nini magenge haya huwalenga wasichana. Lengine la kuvunja moyo ni tohara kwa wanawake, ama ukeketaji. Mtu anaweza kuandika kitabu kizima juu ya ukeketaji barani Afrika.

Kwa kweli, tangu kuadhimishwa rasmi kwa siku hii yapata miaka 45 iliyopita, siku hii inafaa kutumiwa kulaani madhila ambayo wanawake wanaendelea kupitia, badala ya kuwa siku ya sherehe.