1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Swali dogo, athari kubwa

Marcel Fürstenau/Mohammed Khelef18 Agosti 2016

Serikali ya Ujerumani inaonekana kutaka kujitenganisha na waraka wake unaosemekana kuishutumu Uturuki kuwa kitovu cha makundi ya kigaidi, lakini Marcel Fürstenau anaona hata kujitenganisha huko kunazua maswali kadhaa.

https://p.dw.com/p/1Jk7I
Bildkombo Angela Merkel Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/dpa/Sagolj/Zivulovic/Kombo

Hapana shaka, Kansela Angela Merkel anajikuta katika wakati mgumu wakati huu akirudi tena ofisini baada ya mapumziko. Anakutana na ujumbe usiopendeza, suala muhimu sana la uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki. Tuhuma kwamba serikali yake inafahamu – kama haimchukulii – Rais Recep Tayyip Erdogan kuwa muungaji mkono wa makundi ya kigaidi. Hilo laweza kuwa ni matokeo ya tafsiri, lakini angalau ndivyo kilivyofahamu na kutangaza kituo cha televisheni cha serikali, ARD.

Kwa hakika, hadi sasa serikali kuu ya shirikisho imekuwa ikijiepusha kuzungumzia hadharani suala la ukuruba kati ya mshirika wake huyo kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO na ugaidi. Na yumkini inafanya hivyo kwa kuwa jambo hilo halina maslaha nalo, hasa panapohusika suala kubwa zaidi na lenye maslahi ya moja kwa moja na Ujerumani, yaani suala la wakimbizi wanaotaka kuingia barani Ulaya.

Serikali kuu ya shirikisho mjini Berlin inaonekana kuogopa kuwa huenda Rais Erdogan akayatupilia mbali makubaliano baina yake na Umoja wa Ulaya, kuwazuwia wakimbizi. Hilo si jambo lililo mbali na uwezekano, hasa kwa kuzingatia aina gani ya kiongozi Erdogan amejithibitisha.

Kommentarfoto Marcel Fürstenau Hauptstadtstudio
Na Marcel FürstenauPicha: DW/S. Eichberg

Kitu ambacho Kansela Merkel hataki hata kukisikia kwa mbali ni kulazimishwa kukipoteza kile ambacho amekisaka kwa udi na uvumba miaka kadhaa. Na sasa, kwa mujibu wa ARD, waraka wa siri kutoka kwa waziri anayehusika na masuala ya ndani kwenye bunge la Ujerumani, Ole Schröder, unaonekana kumuweka pabaya Kansela Merkel.

Schröder na bosi wake, waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Thomas de Maiziere, wanaonekana kumuweka kansela na mwenyekiti wa chama chao kwenye fadhaa isiyo ya lazima. Na tuhuma zinabakia mikononi mwa waliopokea waraka wa jibu hilo la serikali, yaani chama cha upinzani cha “Die Linke.”

Tuhuma ni kuwa wabunge wa chama hiki cha mrengo wa shoto ni vidomodomo wanaopenda kusikika kwenye vyombo vya habari na hivyo wamekiweka hadharani kile ambacho tangu wanakipokea walishaambiwa kuwa ni jambo la siri. Lakini kwani “uripuaji wa mabomu” kama haya ya kisiasa si ndio sanaa ya makundi yote ya kisiasa duniani.

Lakini kwenye “uripuaji” huu wa sasa, dhamira ya waripuaji inaonekana wazi, kwa sababu chama hiki cha mrengo wa shoto kina mashaka yake na sera ya wakimbizi ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya.

Hata hivyo, swali ni kwa nini taarifa zote hizi za siri ziliwekwa kwenye waraka mmoja huu? Kubwa zaidi ni kwa nini sasa chama hiki kilipewa taarifa hizi, ambazo kila mara huko nyuma upinzani, wakiwemo wale wa chama cha walinzi wa Mazingira, Die Grüne, wamekuwa kinakataliwa na serikali hii hii?

Mwandishi: Marcel Fürstenau
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Caro Robi