Maoni: Trump aongeza joto kwa kupendekeza kusogeza uchaguzi
31 Julai 2020Rais wa Marekani Donald Trump alifanya kila kitu kukanusha kuwa janga la COVID-19 ni hatari. Alidanganya.
Trump alichagua kuulinda uchumi badala ya afya, na athari zikawa mbaya mno. Matokeo yake ni vifo vya zaidi ya watu 150,000 na vinaongezeka – na mporomoko wa kihistoria wa uchumi.
Hali inaonekana kutokuwa na mwisho. Idadi ya visa inaongezeka, kama ilivyo hofu ya raia wa Marekani kuwa wataambukizwa. Hiyo ni hali mbaya kwa biashara na uchumi. Mgogoro wa kiuchumi duniani unaendelea kutokota na nafasi za Trump kuchaguliwa tena zinafifia.
Kama uchumi utaendelea kuporomoka, rais huyu mwenye ahadi kubwa kubwa hatoshinda uchaguzi wa Novemba 3. Tayari yuko nyuma ya mpinzani wake wa Democratic Joe Biden katika uchunguzi wa maoni.
Trump anaendelea kusababisha uharibifu
Lakini kadri mapungufu ya Trump yanavyojitokeza, ndivyo nguvu zake zinavyoendelea kusababisha uharibifu. Baada tu ya habari kuwa pato jumla la ndani la Marekani lilishuka kwa Zaidi ya asilimia 30 katika robo ya pili ya mwaka kutolewa Alhamisi, Trump akapendekeza wazo la kuarishwa uchaguzi akiandika kwenye Twitter.
Kwamara nyingine tena alidai kuwa upigaji kura kupitia njia ya posta ungesababisha udanganyifu, hata ingawa hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai hayo. Hata hivyo hajali. Wala hajali kuwa kutakuwa na sababu chache za msingi za kisheria za kuahirisha uchaguzi kwa sababu ya janga la corona.
Vurugu Zaidi zatarajiwa Novemba
Kadri uchaguzi unavyokaribia, ndivyo inavyokuwa wazi kuwa Trump amejiandaa kuitumbukiza Marekani katika vurugu Zaidi na kudhoofisha misingi yake ya kidemokrasia. Hiyo ndio sababu ya hatua zake za karibuni za kisiasa. Kwa nini aliwatuma maafisa wa serikali kuu mjini Portland? bila shaka sio kutuliza ghasia, bali kuongeza moto na kutanua migawanyiko nchini humo.
Biden na Wademocrat wengine kama vile Bernie Sanders tayari wameonya kuwa Trump hatoondoka bila kupambana.
Kulitumia jeshi katika kutatua ghasia za maandamano nchini Marekani kunatia wasiwasi. Ukweli kwamba warepublican wengi wanaendelea kujitenga na rais huyo labda ni ishara nzuri. Wanaanza kuelewa kuwa hawatakuwa na maisha mazuri kama wataendelea kumuunga mkono, na pia nao watabebeshwa lawama.
/dw/en/trump-ups-the-ante-by-proposing-poll-postponement/a-54386614