Hatimaye ametimiza ndoto yake!!. Heshima na ndoto kubwa na ya mwisho kwa Lionel Messi imetimia baada ya timu yake ya taifa ya Argentina kubeba kombe la michuano ya Kombe la Dunia. Ni kipi kingine anachokihitaji? Hakika sasa anaweza bila ya mashaka yoyote kutambuliwa kama mchezaji bora kabisa wa soka wa muda wote.
Ndio.. Anastahili, ingawa Pele, mchezaji nguli wa zamani wa Brazil aliyeshinda Kombe la Dunia mara tatu bado anasalia kuwa bora zaidi kwa kuwa hakuna aliyeivunja rekodi yake. Lakini hata hivyo soka lilikuwa la tofauti katika kipindi hicho cha mwaka 1958, 1962 na 1970. Messi kwa upande wake amecheza katika kipindi cha ushindani mkali, wenye mechi nyingi, ngumu na zenye shinikizo kubwa.
Soma Zaidi: Argentina yatinga fainali Kombe la Dunia
Ameng'ara katika kipindi chote akiwa uwanjani, ameiwezesha Barcelona kushiriki mara nne michuano ya Klabu bingwa Ulaya ama Champions na ubingwa wa ligi ya Uhispania mara 10. Ameiongoza pia Argentina kwenye michuano ya Copa America mwaka jana. Messi aidha ana rekodi ya kushinda mara saba tuzo ya mwanasoka bora ulimwenguni ya Ballon d'Or.
Messi pia amethibitisha kuwa na uwezo wa kucheza bila ya matatizo yoyote akiwa na klabu tofauti na Barcelona aliyodumu nayo kwa muda mrefu, na hasa baada ya kuisaidia klabu yake ya sasa ya Paris Saint-Germain kuchukua ubingwa wa ligi ya Ufaransa msimu uliopita.
Maajabu yaliyoko kwenye miguu yake.
Lakini sio tu makombe aliyoshinda Messi, bali hata uchezaji aliouonyesha kwenye michuano hii ya Kombe la Dunia, unamaliza moja kwa moja ubishi kwamba yeye ndio bora zaidi kwa sasa. Mamilioni ya watoto kote ulimwenguni wanasema wanavutiwa na soka kwa sababu ya Messi, Kijana mdogomdogo wa umbo, mwenye aibu na maajabu kwenye miguu yake.
Hakufanikiwa kuondoka na kiatu cha dhahabu kwenye michuano hii akizidiwa na Kylian Mbappe wa Ufaransa aliyefunga mabao matatu na kuwaingiza miamba hao katika mikwaju ya penati kwenye mechi ya fainali, ingawa hii haimsumbui sana Messi kwa sababu tayari ameshinda tuzo kadhaa kama mchezaji binafsi kwenye michuano mbalimbali.
Soma Zaidi: Qatar 2022: Argentina, Poland na Australia nazo zafuzu kwa duru ya 16 bora
Pamoja na haya yote, kile chenye uzito zaidi hapa na hasa baada ya machungu ya kuondolewa na Ujerumani katika muda wa ziada mwaka 2014 ni kwamba kwa sasa Messi ni bingwa wa dunia, hata baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Saudi Arabia katika mechi yao ya ufunguzi.
Mnyenyekevu na mwenye furaha wakati wote.
Hapo nyuma, ilisemekana kwamba marehemu Diego Maradona aliyeichezea Argentina ndio alikuwa bora zaidi kiuchezaji, lakini zuio kutokana na matumizi ya dawa za kulevya, balo la "Mkono wa Mungu" na madai ya kujihusisha na magenge ya uhalifu yaliyoko Italia vyote vinamaanisha kwamba Maradona hastahili sifa hii ya kuwa bora zaidi. Ingawa ni kweli Argentina isingeweza kuchukua ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1986 bila bao hilo la Mkono wa Mungu.
Na wakati iliipasa Amerika ya Kusini kusubiri kwa miaka 20, wakati Ulaya ikitawala, sasa Messi ameivunja laana hiyo na kuizuia Ufaransa kulitetea kombe hilo.
Kuna wale ambao bado wanadhani Christiano Ronaldo ndio bora zaidi. Lakini medali ya kombe la dunia zinakosekana kwenye orodha ya mafanikio yake. Tusisahau pia kulinganisha namna Messi alivyoondoka Barcelona kwa machozi, simanzi na unyenyekevu mkubwa, tofauti na Ronaldo aliyeondoka Manchester United, Real Madrid na Juventus kwa kiburi, majivuni na aliyejawa na ubinafsi.
Ni washindi wa Kombe la Dunia. Na mechi ya mwisho ya michuano hiyo imemuweka Messi kwenye kiwango cha juu kabisa cha soka.
Sikiliza Zaidi: