Maoni: Uchaguzi wa Kenya 2022 mageuzi bado yanahitajika
16 Agosti 2022Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Kenya yametangazwa, ambapo naibu wa sasa wa rais, William Ruto, aliyewahi kutuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na anayeshukiwa kupata utajiri wake mkubwa kwa njia za kifisadi, ametangazwa kuwa rais mteule katika hali ya utata.
Ni mgeuko wa kufadhaisha kwa kile ambacho awali kiliwahi kuonekana kama uchaguzi wa wazi kabsia kuwahi kutokea nchini Kenya. Baada ya siku moja ya uchaguzi ambao kwa kiasi kikubwa haukuwa na matatizo, takribani wiki nzima ya kuhisabu na kujumuisha matokeo, na fomu za matokeo zilizotumwa mtandaoni kwa uwazi kabisa ili kila mtu azione, katika dakika zake za mwisho mchakato huu ukageuka kuwa vituko na vitimbi.
Sehemu kubwa ya makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), chombo kinachosimamia uchaguzi huo, walijitenga na matokeo kwenye siku ya mwisho, wakiuita mchakato wenyewe kuwa na utata. Miongoni mwao alikuwa naibu mkuu wa tume hiyo, ambaye kabla ya hapo alikuwa ndiye anayeonekana kwenye ukumbi wa majumuisho wa Bomas of Kenya, Nairobi, akitangaza matokeo ambayo sasa anaonekana kuyatilia shaka.
La kukhofisha zaidi kuliko yote, wakati ujumuishaji matokeo ukienda kwa mwendo wa jongoo, Wakenya walibakia majumbani mwao huku skuli na maduka yakifungwa. Kwamba haya yalikuwa matunda ya uchaguzi ambao, hadi kuelekea utangazwaji wa matokeo ya mwisho ya urais, ulikuwa umesifiwa kuwa somo la uwazi, ni jambo linalosumbua.
Kipi kilikwenda sivyo?
Nadhani kwamba tatizo lilikuwa kwamba hata kama ilisafisha yote, wengine waliokuwa na mtazamo hasi kuhusu mchakato huu hawakuwa wamefanya hivyo. Kwa mfano, vyombo vya habari, ambavyo vilikuwa vimweahidi ujumuishaji ulio huru, ghafla vilisitisha kazi hiyo bila ya kutoa maelezo, hivyo kuandaa mazingira ya kila aina ya wasiwasi.
Wengine walisema ujumuishaji wa vyombo vya habari umedukuliwa na wengine walisema kwamba fomu za kwenye mtandao wa IEBC - ambao vyombo vya habari viliutegemea kufanya hisabu zao - ulikuwa umechezewa. Ushahidi mwepesi wa hili ulitolewa lakini ukimya wa vyombo vya habari ukaruhusu uvumi kusambaa.
Zaidi ya hapo, muungano wa Azimio la Umoja, ambalo mgombea wake Raila Odinga, ameshindwa kwa kura chache, kwa siku kadhaa ulikuwa na mawakala wake kwenye ukumbi huo wakati IEBC ikiendelea na uthibitishaji wa matokeo ili kuangalia uhalali wa fomu ambazo zingelitumika kutangaza matokeo ya mwisho.
Hakuna wakati wowote, hata wakati matokeo yalipokuwa yakitangazwa hadharani na fomu kuwekwa mtandaoni kwa kile mtu kuona, walipolalamika. Na hata baada ya kuyakataa matokeo, muungano huo haukusema chochote juu ya nia yake - ama endapo ungeliyapinga matokeo hayo mahakamano au ungelitumia njia nyengine kulitatuwa jambo hilo.
Marakibisho yashuke kwa wananchi
Vile vile, makamishna wanne waliojienguwa walishindwa kutoa sababu za kujitenga kwao na matokeo, zaidi ya shutuma tupu na za vijembe kwamba kuna utata. Hakuna moja kati ya haya kinachosema kwamba vyombo vya habari, wanasiasa na makamishna hawana sababu inayofaa kwa upinzani wao wa matokeo haya.
Lakini kwa Wakenya ambao kwa zaidi ya muongo mmoja wamekuwa wakitaka uwazi wa IEBC, ni vigumu kwao sasa kugeuka na kuona kwamba ni taasisi na watu wale wale ambao wangelifaidika na uwazi kama huo ndio sasa walio watetezi wa giza.
Kama kuna kitu ambacho Wakenya wanapaswa kujifunza kutokana na uchaguzi huu ni kwamba uwazi kutoka kwa mamlaka za dola zinazoendesha uchaguzi, japokuwa ni wa lazima, lakini hautoshelezi ikiwa haukuendana na uwazi kama huo kwa upande wa watu na taasisi zinazohusika na mchakato wenyewe.
Ndani ya kipindi cha miaka 15 iliyopita tangu uchaguzi wa 2007 uliozuwa ghasia ziliopelekea zaidi ya watu 1,300 kuuawa na maelfu kwa maelfu kuyakimbia makaazi yao, juhudi za kuufanyia mageuzi mfumo wa uchaguzi zimejikita zaidi kwenye haja ya kupunguza ushawishi wa vyombo vya dola, ambavyo kihistoria ndivyo vimekuwa vikibeba dhamana kubwa zaidi ya ghadia na wizi wa kura ulioshuhudiwa kwenye chaguzi zilizopita.
Sasa juhudi hizo lazima zitanuliwe na kuwajumuisha watendaji wengine kwenye mfumo wa uchaguzi.