Serikali yashangilia ushindi wa ''Hapana''
6 Julai 2015Wapiga kura wengi wa Ugiriki wameukataa mpango wa hivi karibuni wa hatua kali za kubana matumizi pamoja na kufanyika mageuzi kama ilivyopendekezwa na wakopeshaji wa kimataifa katika kura ya maoni iliyopigwa jana Jumapili. Hata hivyo, ingawa mapendekezo hayo hayako tena katika meza ya mazungumzo tangu yalivyovunjika siku tisa zilizopita, matokeo hayo yanaonekana kama tafsiri. Serikali inataka kupata faida kutokana na matokeo hayo.
Idadi kubwa ya wananchi wa Ugiriki wamekataa hatua za nyongeza za kuimarisha uchumi wa nchi hiyo na kuwafanya kulazimika kuendana na sharti la kanda ya sarafu ya Euro, hivyo kuunga mkono mbinu na siasa za serikali ya Waziri Mkuu Alexis Tsipras. Serikali ya muungano ya mrengo wa kushoto ya Ugiriki imetumia miezi mitano kujadili mapendekezo hayo, kabla ya kujiondoa hivi karibuni.
Je sarafu ya Drachma ianzishwe tena kama alama ya heshima kwa demokrasia ya Ugiriki? Kwa bahati mbaya, hali ni ngumu zaidi ya hapo. Watu walipanga foleni ndefu kuuzunguka mji wa Athens hapo jana, lakini siyo kwenye vituo vya kupigia kura, bali kwenye mashine za kutolea pesa.
Tsipras azinoa silaha zake
Kila unapoanza usiku wa manane, watu wanajaribu kutoa pesa wanazohitaji. Ni asilimia 60 tu ya wapiga kura ndiyo walishiriki kwenye kura hiyo ya maoni, ingawa chama cha Syriza kilihamasisha kadri kilivyoweza, hata jamii ya Waturuki wachache wa Thrace. Isitoshe Wagiriki wamechoshwa na wasiasa wao na wamekuwa wakijaribu kutafuta mbinu za kuweza kuishi.
Lakini wakati huo huo, serikali ya Tsipras inasherehekea ushindi wa ''Hapana'' na kuonyesha matumaini. Katika siku chache zilizopita, Ugiriki imekuwa ikidai kwamba itafikia makubaliano mapya ndani ya saa 48. Ikawa thabiti zaidi jana Jumapili. Timu ya Tsipras ilitangaza kuwa imepata silaha mpya katika mazungumzo, yaani matokeo ya kura ya maoni.
Hatua hiyo imekuja kama nyongeza ya ripoti ya Shirika la Fedha Duniani-IMF iliyotolewa Alhamisi iliyopita, iliyoeleza kuwa deni la Ugiriki halikuwa endelevu na kwamba vyote viwili, kuongezwa kwa deni na msahama wa madeni vinahitajika.
Lakini, iwapo wakopeshaji wataendelea kubakia kutoridhishwa, hatua madhubuti zimechukuliwa jana usiku. Serikali ya Ugiriki ilizuia kiasi cha Euro bilioni 10 kuingizwa katika masanduku salama ya benki. Inataka kujua kama fedha hizo ni mkusanyiko wa fedha zilizopatikana kutokana na kukwepa kulipa kodi.
Mungu awalinde watu wa Ugiriki kutoka kwa wanasiasa wao.
Mwandishi: Spiros Moskovou/DW
Tafsiri: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Iddi Ssessanga