Ugiriki: Watoto kuondoka kwenye kambi ni ahadi iliyovunjika
7 Aprili 2020Watoto hao wamo hatarini,wametelekezwa,hawana ulinzi, wana majeraha ya moyoni na wakati wowote wanaweza kutendewa ukatili. Maalfu ya watoto hao wakimbizi wapo kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ugiriki bila ya wazazi wao. Mwezi uliopita Ujerumani pia ilitoa ahadi ya kuwachukua baadhi ya watoto hao hata hivyo mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Wote wanakubaliana kwamba hali kwenye kambi za wakimbizi nchini Ugiriki ni ya maafa makubwa .Hali hiyo ni kinyume cha hadhi ya mwanadamu na inakiuka sheria zinazopaswa kuwalinda watoto. Pana haja ya kuwajibika kuchukua hatua. Serikali ya Ujerumani haisemi kwa uhakika ni watoto wangapi itakuwa tayari kuwachukua miongoni mwa takriban watoto 1600 walioahidiwa kusaidiwa na serikali za nchi nane za Umoja wa Ulaya.
Halmashauri ya Umoja wa Ulaya inawajibika juuya kuwagawanya watoto hao miongoni mwa nchi wanachama. Kinachotakiwa sasa ni mshikamano. Wabunge 50 wa vyama ndugu vya CDU na CSU wametoa mwito kwa rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen wa kuwaondoa watoto hao kutoka kwenye kambi ya wakimbizi nchini Ugiriki na kuwapeleka kwenye nchi nyingine za Umoja wa Ulaya.
Wabunge hao wamesema katika barua waliyoandika kwamba, hali ya kutisha kwenye kambi hizo haiwezi kuendelea bila ya kuwagusa watu wote barani Ulaya . Wabunge hao pia wametanabahisha kuwa hali kwenye kambi za wakimbizi ilikuwa mbaya hata kabla ya kulipuka janga a maambukizi ya virusi vya Corona. Na jee sasa mazingira yatakuwaje endapo janga hilo litalipuka kwenye kambi hizo?
Kansela wa Ujerumani hajawahi kuungwa mkono na wajerumani kama ilivyo katika wakati huu mgumu wa janga la corona! Mshikamano huo unapaswa kumpa moyo na uthabiti. Hali ya sasa siyo ile ya mwaka 2015 ambapo serikali ya Ujerumani iliwapokea maalfu kwa maalfu ya wakimbizi.
Serikali ya Ujerumani haina haja ya kuwa na hofu juu ya kukipa mtaji wa propaganda chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD, ati kwa sababu ya kuchukua hatua za kibinadamu ili kuwasaidia watoto hao. Ni watoto wachache tu wanaohitaji kulindwa na kusaidiwa. Pana haja ya kuchukua hatua za haraka.!
Chanzo:/ LINK: http://www.dw.com/a-53028547