1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan apewa onyo

Admin.WagnerD19 Julai 2016

Wahariri wa magazeti wanatoa maoni juu ya hofu ya kurudishwa adhabu ya kifo nchini Uturuki.Pia wanatoa maoni juu ya dawa za kuongeza nguvu za wanamichezo

https://p.dw.com/p/1JRNb
Recep Tayyip Erdogan Türkei Istanbul
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/T.Bozoglu

Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anasema kauli anazozitoa Rais wa Uturuki Erdogan juu ya kutaka adhabu ya kifo irejeshwe nchini humo siyo jambo la kushangaza.

Mhariri anasema ni wazi Erdogan anajua kwamba kurudishwa adhabu hiyo nchini mwake maana yake ni kusahauliwa kabisa kwa mazungumzo juu ya nchi yake kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hata hivyo katika siku za hivi karibuni Erdogan ameitumia kila fursa ili kuuonyesha Umoja wa Ulaya kuwa yeye ni kiongozi imara.

Mhariri wa gazeti la "Landeszeitung" anasema Rais wa Uturuki anaushikilia mjadala juu ya kuiondoa nchi yake kutoka kwenye utaratatibu wa utawala wa kisheria.

Mhariri huyo anawataka viongozi wa Umoja wa Ulaya wajiulize kwa nini Erdogan ameanzisha kampeni kubwa ya kuwalenga polisi na wanasheria fulani. Mhariri wa "Landeszeitung" anatuhumu kwamba Erdogan tayari alikuwa nayo majina ya watu hao katika mashubaka yake.

Umoja wa Ulaya hautakubali adhabu ya kifo

Naye mhariri wa "Südwest" anasisitiza katika maoni yake kwamba ikiwa adhabu ya kifo itarejeshwa nchini Uturuki hapatafanyika mazungumzo juu ya nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Ulaya. Viongozi wengi wa nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na wa Marekani wameelezea misimamo yao wazi na kwa haraka.

Mhariri wa gazeti la "Südwest" anasema baada ya jaribio lililoshindikana la kuiangusha serikali nchini Uturuki, Rais Erdogan amepoteza vipimo vyote!

Hata hivyo kiongozi huyo hana budi atambue kwamba katika Umoja wa Ulaya yapo maadili yanayotumika na kwamba nchi yoyote inayotekeleza adhabu ya kifo haina chake katika jumuiya hiyo.

Wanamichezo wote wa Urusi hatarini kuachwa nje

Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anazungumzia juu ya ripoti ya Shirika la kupambana na dawa za kuongeza tija ya wanamichezo duniani - WADA .

Uwanja wa michezo wa Sochi
Uwanja wa michezo wa SochiPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba ripoti ya WADA inabainisha kuwa udanganyifu wa kutumia dawa za kuongeza nguvu za wanamichezo ulifanyika kwa ridhaa ya serikali nchini Urusi.

Na sasa siku chache kabla ya mashindano ya Olimpiki kuanza nchini Brazil, Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, IOC inapaswa kuamua iwapo wanamichezo wa Urusi washiriki au wabakie nyumbani.

Mhariri wa "Hannoversche Allgemeine" anasema ikiwa kamati hiyo itawafungia wanamichezo wa Urusi, huo utakuwa uamuzi wa kijasiri kwani ni kwa njia hiyo kwamba imani ya watu itarejea tena katika michezo.

Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Flensburger" anaeleza kwamba mkasa wa Urusi unafichua mengi juu ya medani ya michezo duniani. Fedha nyingi na umaarufu ni mambo yanayowafanya wanamichezo watumie njia haramu. Na ndiyo sababu tija inayooneshwa na vijana katika kukimbia, kuogelea au kuruka, siyo tena jambo la kulistaajabia bali ni la kulitilia mashaka!

Mwandishi:Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Josephat Charo