Maoni ya wahariri juu ya Bin Laden,Snowden na neema kwa Latvia
10 Julai 2013Gazeti la "Südddeutsche" linaiangalia ripoti ya tume iliyofanya uchunguzi nchini Pakistan. Tume hiyo imebainisha kwamba kutokana, na uzembe wa idara za usalama iliwezekana kwa kiongozi wa mtandao wa Al-Kaida Osama bin Laden kuishi nchini humo kwa muda wa miaka tisa bila ya kujulikana. Mhariri wa gazeti la "Süddeutsche"anasema ripoti hiyo ni ya ujasiri lakini haikutolewa katika wakati unaostahili.
Gazeti la"Münchner Merkur" pia linaizungumzia ripoti ya tume ya Pakistan kwa kutilia maanani kuwepo kwa Osama Bin Laden nchini humo hadi pale alipouawa.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ya badala ya kukataliwa, Osamba Bin Laden alikuwa anastaajabiwa nchini Pakistan . Aliweza kuishi nchini humo katika msingi wa mkataba wa kauli. Bin Laden alijua kwa nini aliichagua Pakistan.Wenyeji wake pia walijua kwa nini.Kadhalika waliokuwa wanamwinda-yaani Marekani, yumkini hawakuwa kizani kabisa juu ya kuwepo kwa Obana Bin Laden nchini Pakistan.
Latvia kujiunga na Ukanda wa sarafu ya Euro:
Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wametoa idhini kwa Latvia ya kujiunga na Ukanda wa sarafu ya Euro. Nchi hiyo itaanza kuitumia sarafu ya Euro mnamo mwezi wa januari,mwaka ujao. Mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine" anasema hizo ni habari nzuri na anaeleza: Kujiunga kwa Latvia na Umoja wa sarafu ya Euro kunathibitisha kwamba Umoja huo unastawi, tofauti na utabiri wa watu fulani wa hapo awali juu ya kusambaratika kwa jumuiya hiyo.Jumuiya ya Euro inaimarika na huenda Lithuania nayo ikajiunga mnamo mwaka wa 2015. Kustawi kwa jumuiya hiyo kuinaimarisha nguvu za nchi zinazotaka nidhamu ya bajeti na ustawi wa uchumi .
Wataka kumsaidia Snowden:
Gazeti la "Straubinger Tagblatt" bado linauzingatia mkasa wa Edward Snowden, wakala wa zamani wa Shirika la ujasusi la Marekani la CIA, aliefichua kashfa ya kupelelezwa simu na mitandao ya watu. Gazeti hilo linasema katika maoni yake kwamba wale wanaotaka kumsaidia,Snowden wana shabaha fulani. Gazeti hilo linaeleza kwamba nchi zinazosema zipo tayari kumsaidia Snowden hazina malengo ya kutetea uhuru wa vyombo vya habari wala ulinzi wa faragha ya wananchi. Lengo la nchi hizo ni kumuumbua Rais Obama na zinataka kuzipata habari zenye thamani kubwa zilizomo katika mikono ya Snowden.
Mwandishi: Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri: Mohammed Khelef