1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Chavez na juu ya umasikini Ujerumani

Abdu Said Mtullya7 Machi 2013

Wahariri wanatoa maoni juu ya Hugo Chavez na pia wanaizungumzia ripoti juu ya hali ya umasikini nchini Ujerumani iliyotolewa jana

https://p.dw.com/p/17shp
Elena Frias (3rd L), mother of late Venezuelan President Hugo Chavez, stands with her other sons next to his coffin during a wake at the military academy in Caracas March 6, 2013, in this picture provided by the Miraflores Palace. Authorities have not yet said where Chavez will be buried after his state funeral on Friday. REUTERS/Miraflores Palace/Handout (VENEZUELA - Tags: POLITICS OBITUARY) ATTENTION EDITORS - THIS IMAGE HAS BEEN SUPPLIED BY A THIRD PARTY. IT IS DISTRIBUTED, EXACTLY AS RECEIVED BY REUTERS, AS A SERVICE TO CLIENTS. FOR EDITORIAL USE ONLY. NOT FOR SALE FOR MARKETING OR ADVERTISING CAMPAIGNS
Watu wa Venezuela waomboleza kifo cha ChavezPicha: REUTERS

Juu ya Chavez gazeti la"Braunschweiger"linasema kiongozi huyo alipata mafanikio katika sekta ya kijamii.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba Chavez aliutumia utajiri wa mafuta kuziendeleza huduma za afya na elimu Lakini pia aliwashirikisha watu wake katika faida zilizozotokana na mauzo ya mafuta.Pamoja na kasoro zilizokuwamo katika mfumo wake wa uongozi,jambo moja,tunapaswa kulikubali,kwamba mageuzi,aliyoyaita,mapinduzi yana mashiko.


Mhariri wa gazeti la"Augsburger Allgemeine"hakubaliani na sifa hizo.Anasema Chavez aliuangusha uchumi wa Venezuela.Mhariri huyo anauliza vipi mtu anaweza kuiporomosha nchi yenye utajiri mkubwa kama Venezuela? Chavez aliwagawanya watu wake. Sera zake za kuwasaidia wadhulumiwa zilienda sambamba na kuwapiga vita watu wa matabaka ya juu.Chavez aliutifua msingi wa uchumi wa matabaka hayo na pia alizibana haki za msingi za binadamu.

Umasikini nchini Ujerumani

Ripoti juu ya hali ya umasikini nchini Ujerumani ilitolewa jana na serikali huku kukiwa na madai kutoka kwa vyama vya upinzani na vyombo vya habari,kwamba ripoti hiyo ilichakachuliwa.Wahariri wa magezeti wametoa maoni yao juu ya ripoti hiyo na hali ya umasikini nchini Ujerumani kwa jumla.

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linasema umasikini ni jambo la uwiano,au takwimu ,katika nchi tajiri sana,kama Ujerumani.Tishio kubwa la kutumbukia katika umasikini ni ukosefu wa ajira.Madhali idadi ya vijana wasiokuwa na ajira nchini Ujerumani ni ya chini kabisa kulinganisha na nchi nyingine barani Ulaya,lawama zinazotolewa na wanasiasa wa upande wa upinzani ni kama mshale uliopotea njia!

Sababu zichunguzwe:

Naye mhariri wa gazeti la"Märkische Allgemeine"anawashauri wanasiasa juu ya kuzichunguza sababu za umasikini nchini Ujerumani.Mhariri huyo anasema badala ya kuzungumzia juu ya ubabaishaji wa takwimu na kujaribu kutoa picha ya kutisha juu ya umasikini, ripoti iliyotolewa na serikali inapasa kuwa wasaa kwa wanasiasa, wa kuyajadili mazingira yanayosababisha umasikini.Mhariri wa gazeti hilo anasema "Sote tunataka pawepo masikini wachache kwa kadri itakavyowezekana nchini Ujerumani.Lakini hatujakubliana juu ya njia ya kulifikia lengo hilo."

Mhariri wa"Freie Presse"anazitaja baadhi ya sababu za umasikini nchini Ujerumani kwa kueleza kuwa sera za kodi na za kijamii, za miaka 10 iliyopita zimewafanya matajiri wazidi kuwa tajiri, na masikini wazidi kuwa masikini.Masikini,ni masikini siyo kutokana na ukosefu wa fedha bali pia hawana usalama wa kijamii,na wala hawashiriki katika michakato ya kisiasa na kijamii.Watu waliomo katika hali ngumu za kijamii,wanatambulika kwa mapungufu ya kielimu ,na siyo tena kwa tafauti za mapato.Inavyoekelea Serikali ya Ujerumani bado haijalitambua hilo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Yusuf Saumu