1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Konrad Adenauer

Abdu Said Mtullya6 Juni 2013

Wadau wa mashirika kadhaa wamehukumiwa vifungo nchini Misri.Na Wakfu wa Ujerumani "Konrad Adenauer" umefungwa nchini humo. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao.Abdu Mtullya anatuletea maoni hayo

https://p.dw.com/p/18ksZ
Hakimu akitoa hukumu dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali mjini Kairo
Hakimu akitoa hukumu dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali,mjini KairoPicha: picture-alliance/dpa

 Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linasema hukumu za vifungo zilizotolewa na mahakama ya nchini Misri zinaonyesha jinsi uhusiano baina ya Misri na Ujerumani  ulivyoshuka na kufikia kiwango cha chini.

Mhariri huyo anakumbusha juu ya mkataba uliofikiwa baina ya Ujerumani na Misri wa kuwapa wawakilishi wa Ujerumani ulinzi wa kisheria nchini Misri.Lakini serikali ya Misri imeupuuza mkataba huo wa kuilinda asasi ya Ujerumani ya kutetea demokrasia nahaki za raia.

Itikadi kali:

Mhariri wa "Hannoversche Allgemeine" anamlenga Rais Mursi katika maoni yake na anasema lengo la Misri ni kuelekea katika njia ya Uislamu wa itikadi kali.

Naye mhariri wa gazeti la "Cellesche" pia anamlenga Rais Mursi katika maoni yake na anasema Rais Mursi mwenyewe haoni iwapo nchi yake inaweza kunufaika na sampuli ya demokrasia ya nchi za magharibi. Mhariri huyo anaeleza kwamba hatua kama hiyo ya kuyaandamana mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ilichukuliwa na watawala wa Urusi wanaoifuata misingi ya demokrasia wanayoijua wao tu. Gazeti la "Südwest-Presse" linasema ni vizuri kwa mashirika ya nchi za magharibi kujiingiza katika harakati za kuijenga jamii mpya ya Misri.

Ndege zisizokuwa na rubani:

Suala lingine linalozingatiwa na wahariri wa magazeti linahusu mradi wa ndege zisizokuwa na rubani. Suala hilo limezua mzozo mkubwa nchini Ujerumani na waziri wa ulinzi ameyajibu maswali ya wabunge juu ya mradi wa ndege hizo.

Ujurumani ilikuwa na mpango wa kutengeneza ndege yake aina ya "Euro Hawk," na ilitumia fedha nyingi lakini mradi huo haukuweza kuota mbawa.

Lakini gazeti la"Frankfurter Allgemeine" linatetea uwepo wa ndege hizo,kwa kusema kwamba ndege hizo zinawapa wanajeshi uwezekano wa kuwapeleleza adui na  hatimaye kupambana nao,bila ya kuwapo hatari ya nchi kuwapoteza askari wake .

Ikiwa Ujerumani itaamua kuwapeleka askari wake vitani nchi za nje,askari hao watapaswa kuwa na vifaa madhubuti, na bila shaka ndege hizo zisizokuwa na rubani zitapaswa ziwe sehemu ya vifaa hivyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman