1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mauaji ya Armenia kuitwa ya halaiki

Admin.WagnerD1 Juni 2016

Wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya mvutano baina ya Uturuki na Ujerumani kuhusu mauaji ya watu wa Armenia yaliyotokea miaka mia moja iliyopita. Pia wanatoa maoni juu ya biashara ya silaha na Saudi Arabia

https://p.dw.com/p/1IyHP
Mauaji ya halaiki ya watu wa Armenia
Mauaji ya halaiki ya watu wa ArmeniaPicha: picture alliance/CPA Media

Bunge la Ujerumani linatarajiwa kuamua juu ya istilahi itakayotumika kuyaainisha mauaji ya watu wa Armenia yaliyofanywa na majeshi ya utawala wa Osman miaka mia moja iliyopita.

Jee mauaji hayo yalikuwa ya halaiki? Rais wa Uturuki amesema ikiwa Bunge la Ujerumani litayaita mauaji hayo kuwa ya kimbari uhusiano utaharibika baina ya Ujerumani na Uturuki.

Mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anasema azimio litakalopitishwa na Bunge la Ujerumani litakuwa ishara ya kutahadharisha juu ya kutoisahau historia.

Erdogan ndiye anaelengwa

Mhariri huyo anaeleza kwamba kuyaita mauji hayo kuwa ya kimbari ni kukumbusha juu ya maafa yaliyowakumbuka watu wa Armenia.

Hata hivyo mhariri wa gazeti la "Hannoversche Allgemeine" anasema ni jambo la kusikitisha kwamba mjadala huo unamlenga zaidi Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan.Na kwa hivyo pana hatari ya watu wa Armenia kusahauliwa.

Naye mhariri wa "Landeszeitung" anasema Bunge la Ujerumani litapitisha hapo kesho(Alhamisi) azimio la kuyatambua mauaji ya watu wa Armenia kuwa ni ya halaiki.

Anasema ni kweli kwamba wakati siyo mujarabu kutokana na ukweli kwamba Ujerumani inaitegemea Uturuki juu ya suala la wakimbizi.

Lakini anahoji kuwa ni sahihi kwa Bunge la Ujerumani kutamka wazi juu ya unyama uliofanywa kwa watu wa Armenia mnamo mwaka 1916.

Biashara na Saudi Arabia

Gazeti la "Volksstimme" linazungumzia juu ya biashara ya silaha na Saudi Arabia.

Biashara nyeti ya silaha na Saudi Arabia
Biashara nyeti ya silaha na Saudi ArabiaPicha: dapd

Mhariri wa gazeti hilo anasema kila mara inapobidi kuuza silaha kwa nchi hiyo mijadala mikali inazuka nchini Ujerumani. Lakini anasema sasa suluhisho limepatikana.

Mhariri huyo anaeleza kuwa biashara ya silaha na Saudi Arabia wakati wote ni suala nyeti katika sera ya uchumi na ya nje ya Ujerumani. Kwa kawaida Ujerumani haiuzi silaha katika maeneo ya migogoro. Lakini mhariri anatilia maanani kuwa sera hiyo haikutekelezwa kwa uthabiti kuhusu Saudi Arabia.Na sasa mjadala mkali unaendelea juu ya iwapo kuiuzia Saudi Arabia vifaru na mashua za kivita za kisasa.

Hata hivyo gazeti linasema ghafla suluhisho limepatikana.Saudi Arabia sasa haitaki kununua silaha kutoka Ujerumani.Imechoshwa na mijadala hiyo.

Gazeti la "Mitteldeutsche" linazungumzia juu ya vikwazo dhidi ya Urusi.Linaeleza kwamba wafanyabiashara na wakulima wa Ujerumani wanataka kufanya biashara tena na Urusi.

Kutokana na matatizo yanayowakabili wakulima, yaliyosababishwa na vikwazo dhidi ya Urusi, chama cha mrengo wa kulia kinachowapinga wahamiaji,AfD kinaitumia hali hiyo kijijengea umaarufu nchini. Kwa hivyo ni sawa kuzungumzia juu ya kulegeza au hata kuviondosha vikwazo hivyo.

Lakini gazeti linasisitiza kwamba inapasa kukumbuka kuwa Urusi imewekewa vikwazo hivyo kwa sababu ya mgogoro wa Ukraine na kwa sababu imeliteka jimbo la Krimea.

Mwandishi:Mtulla abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Iddi Ssessanga