1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Misri na mvutano baina ya Ulaya na Marekani

Abdu Said Mtullya2 Julai 2013

Wahariri hao wanatoa maoni juu ya Misri,mvutano baina ya Marekani na nchi za Ulaya kuhusiana na kupelelezwa kwa nchi hizo, na vile vile wanazungumzia juu ya kujiunga kwa Croatia na Umoja wa Ulaya

https://p.dw.com/p/1907F
Maandamano ya kumpinga Rais Mohammed Morsi nchini Misri
Maandamano ya kumpinga Rais Mohammed Morsi nchini MisriPicha: picture-alliance/AP

Gazeti la"Hannoversche Allgemeine" linazungumzia juu ya matukio ya nchini Misri. Mhariri wa gazeti hilo anaizingatia hasa kauli iliyotolewa na jeshi la nchi hiyo ya kutishia kuingilia kati. Anasema Majerali wa Misri wanataka kulazimisha mambo yasiyowezekana,yaani pande zinazopingana zitafute mwafaka au hata ikiwezekana pande hizo ziunde mseto mkubwa kwa manufaa ya Misri.

Naye mhariri wa gazeti la "Nürnberger" anasema kuwa Rais Morsi amefanya makosa katika sera inayolihusu jeshi la nchi yake.

Mhariri huyo anaeleza kwamba mara tu baada ya kuingia madarakani Rais Morsi alianza kufanya mabadiliko katika jeshi. Lakini hakufanikiwa kama jinsi inavyoweza kushuhudiwa sasa. Yumkini ameshindwa kuyakata kabisa mashikamano baina ya jeshi na mfumo wa hapo zamani wa Mubarak.

Gazeti la "Hessische Niedersächsiche Allgemeine" linasema mizizi ya matatizo ya Misri imeenda chini sana, kinachojitokeza sasa ni dalili tu za matatizo hayo.Na kwa hivyo matatizo hayo yaliyomo katika kizungumkuti yanaweza kutatuliwa na taasisi moja tu. Nalo ni jeshi.

Marekani na Ulaya zavutana:

Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linatoa maoni juu ya mvutano baina ya Marekani na washirika wake wa Ulaya uliosababishwa na ujasusi uliofanywa na mashirika ya Marekani. Gazeti hilo linatahadharisha kwa kusema kwamba mashirika ya ujasusi ya Marekani, yamekuwa kama yamepagawa katika shughuli za upelelezi wa nchi za Ulaya na hasa Ujerumani kiasi cha kuuhatarisha urafiki baina yake na nchi za Ulaya.Upelelezi wa mashirika hayo hauna uhusiano na juhudi za kupambana na ugaidi. Sasa pana sababu ya kutokea hali ya kutoaminiana baina ya Marekani na washirika wake wa Ulaya.

Croatia yajiunga na Umoja wa Ulaya:


Gazeti la "Braunschweiger" linazungumzia juu ya Croatia kujiunga na Umoja wa Ulaya na linaitathmini hatua hiyo kuwa ni mchango mkubwa katika kudumisha amani. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kwamba kwa muda wa miaka 10, yamekuwa yanafanyika mazungumzo juu ya Croatia kujiunga na Umoja wa Ulaya. Hatua hiyo inalisogeza bara la Ulaya mbele katika lengo la kuutekeleza mradi wa amani barani Ulaya. Mkakati wa kuziingiza nchi zaidi za kanda ya kusini mashariki mwa Ulaya katika Umoja wa Ulaya,ndiyo njia ya kudumisha amani katika kanda hiyo ya Balkani. Croatia itatoa mfano kwa nchi nyingine za kanda hiyo.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman