1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya ushindi wa Muhammed Mursi

Abdu Said Mtullya25 Juni 2012

Wahariri wasema Muhammed Mursi atakabiliwa na changamoto kubwa katika kuitekeleza agenda yake kutokana na ukinzani wa wanajeshi.

https://p.dw.com/p/15Krc
Rais mpya wa Misri Muhammed Mursi
Rais mpya wa Misri Muhammed MursiPicha: AP

Juu ya ushindi wa Muhammed Mursi nchini Misri gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linasema ni vigumu kuwapongeza Wamisri kwa ushindi wa mwanasiasa huyo wa chama cha Udugu wa Kiislamu. Linaeleza kuwa Mursi anapaswa kuwaleta Wamisri pamoja na kuleta maridhiano nchini. Lakini yeye ni mwanachama wa chama cha Udugu wa Kiislamu na kwa hivyo siye mtu ambaye anaweza kuaminika na wakristo au Wamisri wanaotaka siasa na dini zitenganishwe.

Gazeti la "Südwest Presse  pia limeandika juu ya Misri baada ya Muhammed Mursi kutangazwa mshindi wa duru ya pili ya uchaguzi. Gazeti hilo linasema baada ya majenerali kutoa amri ya kulivunja bunge,sasa kila kitu ni dhahiri kabisa nchini Misri: majenerali wa Baraza Kuu la kijeshi hawafikirii kuachia mamlaka yaondoke mikononi mwao na kuyakabidhi kwa raia:

Wanajeshi hao wanataka kuelendelea kuwa serikali ndani ya serikali, kama jinsi ambavyo imekuwa kwa ,kipindi cha miaka 60 iliyopita nchini Misri. Utawala wa Mubarak na mihimili yake imethibiti kuwa sugu kuliko ilivyotarajiwa katika muktadha wa kujaribu kuleta mwanzo mpya nchini Misri.

Mhariri wa gazeti la "Stuttgarter Zeitung" ana mashaka iwapo Rais mpya wa Misri Muhammed Mursi ataweza  kuyatimiza matarajio ya wananchi wake. Na anaeleza kuwa watu wa Misri wanatarajia mengi kutoka kwa Rais wao mpya. Mursi anapaswa kuufufua uchumi,kupambana na ufisadi na hasa anapaswa kurejesha usalama na utulivu, baada ya ghasia ziizoandamana na harakati za kuleta mapinduzi.Lakini hataweza kuyatekeleza hayo. Ni wazi kwamba atashindwa, kutokana na majenerali kujifanya kuwa waokozi wa Misri.


Mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt" anatoa maoni juu ya mvutano uliozuka baina ya Syria na Uturuki baada ya ndege ya kivita ya Uturuki kutunguliwa na majeshi ya Syria.Katika maoni yake mhariri wa gazeti hilo anatoa mwito kwa viongozi wa Uturuki wa kutumia busara Mhariri huyo anasema litakuwa jambo la busara ikiwa Uturuki itakuwa na utulivu juu ya mkasa huo. Kuangushwa kwa ndege hiyo siyo sababu ya kuanzisha vita. Nchi za mufungamano wa kijeshi wa Nato haziwajibiki kujiingiza kijeshi Syria kwa sababu ya ndege hiyo.

Hata hivyo Rais Assad anapaswa kutambua kwamba ni jambo la hatari kuchezea moto.! Mhariri wa gazeti la "Flensburger Tageblatt" anatilia maanani kwamba kwa muda mrefu Uturuki imekuwa inalalamika juu ya himaya yake kukiukwa na Syria, na kwamba  nchi za Nato tayari zimeshafikiria juu ya kuchukua hatua za kijeshi. Ni kweli kwamba kwa sasa nchi za Nato hazina nia ya kupitia njia hiyo, lakini kwa kadri utawala wa Assad unavyoendelea kuwaua wananchi wake,ndivyo njia hiyo inavyozidi kuingia akilini.

Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" pia linatoa mwito kwa Uturuki wa kuwa na utulivu juu ya mkasa wa ndege yake kuangushwa na Syria. Kwani hatua za pupa na kukaanga mbuyu hakutakuwa na manufaa kwa Uturuki yenyewe na wala kwa nchi za magharibi kwa jumla. Mhariri wa gazeti hilo pia amelitaka baraza la Nato  litakalokutana kesho kuujadili mkasa huo wa ndege, kuiunga mkono Uturuki, lakini wakati huo huo baraza hilo liishauri Uturuki kutovuka mipaka katika kuujibu uchokozi wa Syria.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman