Uingereza yachukua hatua Syria
3 Desemba 2015Jambo la kulizingatia hapa, si kuchagua kati ya kuchukua hatua au kutochukua hatua ,bali ni kupambanua baina ya kuchukua hatua na kupotosha.
Kauli hiyo ilitolewa na mwanasiasa mmoja wa chama cha kihafidhina nchini Uingereza baada ya Bunge la nchi hiyo kuyaidhinisha mashambulio ya ndege dhidi ya magaidi wa dola la kiislamu. Yeyem mwenyewe aliupinga mswada huo.
Yapo mambo fulani katika duniani hii yasiyohitaji mjadala. Kwa mfano dunia yetu ingelikuwa nzuri zaidi, laiti wasingelikuwapo magaidi wa dola la kiislamu.
Waziri kivuli wa chama cha Labour Hilary Benn, amewaita magaidi wa dola la kiislamu kuwa ni mafashisti, alipotoa hoja ya kuunga mkono mswada wa serikali juu ya Syria. Na amesema dunia inajua kwamba ni lazima mafashisti watokomezwe
Hata hivyo, mjumbe maarufu wa chama cha kihafidhina, David Davis amesema tangu mfungamano wa nchi zinazoongozwa na Marekani uanze mashambulio ya ndege nchini Syria na Irak mwaka mmoja uliopita, idadi ya wapiganaji walioandikishwa na dola la kiislamu imeongezeka mara mbili.
Amekiri kwamba mashambulio hayo yamewalenga wapiganaji muhimu wa dola la kiislamu na yameipunguza kasi ya magaidi hao, lakini Davis,amesema mashambulio hayo hayajaifikia shabaha inayolengwa- yaani kuwadhoofisha magaidi hao na hitamae kuwatokomeza.
Ndege mbili tatu hazitafua dafu
Ni vigumu kuamini kwamba ndege mbili tatu za Uingereza ambazo tayari zinafayna mashambulio nchini Irak, kwa zaidi ya mwaka mmoja, zitaweza kuibadilisha hali kwa kiwango kikubwa katika eneo linaloshikiliwa na wapiganaji wa dola la kiislamu katika ardhi ya Syria.
Ndege za nchi kadhaa zinafanya mashambulio, ikiwa pamoja na za Urusi na za jeshi la Syria yenyewe. Uamuzi uliopitishwa na Bunge la Uingereza umetokana na haja ya kutaka kutoa ishara tu. Ni sawa na uamuzi uliopitishwa na Bunge la Ujerumani.
Ni sawa kabisa kwa nchi za Ulaya kuonyesha dhamira ya kusimama bega kwa bega na Ufaransa baada ya mashambulio yaliyofanywa na magaidi mjini Paris. Lakini hatua za pupa zinaweza kusababisha hatari.
Ahadi za nchi za magharibi juu ya kuimarisha hatua za kijeshi katika Mashariki ya Kati zinaweza kutumiwa na dola la kiislamu kwa shabaha za propaganda na kuwasaidia katika njama zao za kuwaandikisha wapiganaji zaidi.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesisitiza mara kwa mara, kwamba mashambulio ya ndege dhdi ya dola la kiislamu ni sehemu moja tu ya mkakati kabambe dhidi ya watu hao. Lakini jee huo mpango kamili uko wapi na hasa kuhusu Syria? Licha ya kushtushwa na mashambulio ya mjini Paris, watu wa Uingereza bado wana mashaka juu ya pilika pilika za kijeshi za nchi yao katika karne hii ya 21.
Taliban wamerudi tena baada ya miaka 14 tangu nchi za magharibi ziivamie Afghanistan. Magaidi wa dola la kiislamu wanaishikilia sehemukubwa ya Irak kaskazini .Libya imo katika hali mbaya. Yaliotokea katika nchi hizo hayaonyeshi ushahidi wa kuwepo mikakati thabiti ya muda mrefu.
Mwandishi:Mark Hallam
Mfasiri:Mtullya Abdu
Mhariri:Yusuf Saumu