Maoni:Mwisho wa uhakika wa kisiasa Ujerumani
14 Machi 2016Kamwe haijawahi kutokea kwa wapigaji kura wanaoandamana kuacha alama kubwa kama safari hii. Kwa sababu kwa mara ya kwanza chama cha Alternative für Deutschland, AfD, kimejiimarisha sana katika majimbo ya Baden-Württemberg, Rheinland Pflaz na Sachsen-Anhalt.
Chama cha AfD sasa kiko katika njia nzuri ya kuingia katika bunge la taifa: katika majimbo manane kati ya 16 tayari kuna wabunge wa chama cha AfD. Kwa chama kilichoundwa mwaka 2013 huo bila shaka ni ushindi mkubwa. Ushindi huu haungepatikana kabisa kama si kwa mzozo wa wahamiaji. Kwa sababu mzozo huu unaendelea kwa muda mrefu, na huenda ukazidi kuwa mbaya, chama cha AfD kitaeendelea kupata nguvu.
Kwa ushindi wake chama cha AfD hakilazimiki kufanya mengi zaidi, mbali na kutumia hisia za mabarabarani. Vyama vya kisiasa ambavyo vimekuwepo kwa miaka mingi vimepata ushauri mzuri wa kukabiliana na nguvu mpya ya kisiasa iliyojitokeza. Na kwanza kabisa vinalazimika kufanya mabadiliko kuhusu jinsi ya kushirikiana na chama hicho. Anayekataa mapambano na chama cha AfD, hatilii maanani kauli zilizotolewa mara kwa mara na wapigaji kura. Hatua hiyo ingekuwa ni kiburi, na isiyo stahili katika demokrasia.
Chama hicho kimedhihirisha Jumapili iliyopita kama chama chenye uhai. Katika majimbo yote matatu idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura ilikuwa kubwa zaidi kuliko mwaka 2011. Na kwa hilo watu wote watanakiwa kufurahi, ambao vinginevyo hulalamika juu ya ushiriki mdogo katika siasa.
Kwa namna fulani kansela Merkel ameshinda
Bila shaka uchaguzi huo ulikuwa maandamano ya kupiga kura, uchaguzi wa kupinga sera za Merkel kuhusu wakimbizi. Lakini pia mbali na hayo ulikuwa uchaguzi ambapo watu wenye haiba kubwa walijikakamua na kufaulu kushinda. Winfried Kretschmann wa chama cha Kijani - Die Grüne katika jimbo la Baden-Württemberg na Malu Dreyer cha chama cha Social Democratic, SPD katika jimbo la Rheinland-Pfalz.
Viongozi hawa walishinda licha ya kuunga mkono sera za wakimbizi za kansela Merkel. Matokeo ambayo kwa kuzingatia ushindi wa chama cha AfD yanaweza kuwekwa pembeni. Lakini hata hivyo wanabakia kuwa wakuu wa serikali kwa sababu wameaminiwa na watu waliowawakilisha katika majimbo yao. Hii inaonekana pia kwa Reiner Haseloff wa chama cha Christian Democratic Union, CDU, cha kansela Merkel.
Majimbo matatu, washindi watatu waliotetea nafasi zao na vyama vitatu tofauti. Usimwambie mtu eti chaguzi za Ujerumani zinachosha na zinatabirika. Kila mahala sasa kunaanza mazungumzo magumu ya kuunda serikali za mseto. Ni lazima kutakuwa na vizuizi kati ya vyama vya SPD, CDU, Grünen na FDP. Ndiyo, chama cha FDP nacho pia kinashiriki. Miaka miwili baada ya kukosa uwakilishi katika bunge la Ujerumani Bundestag, wapiga kura wameamua kukiheshimu na kukipa tena kura zao. Kwa bahati nzuri, siasa za kiliberali Ujerumani zina mustakabali mwema. Katika mazingira ya siasa motomoto ambayo Ujerumani inajikuta kwa sasa, ni ya kutuliza sana.
Tutake tusitake Ujerumani itakuwa na mseto wa vyama vya siasa. Chama cha Die Linke ndicho kinachotakiwa kuwa na wasiwasi mkubwa kwa kuwa kimepoteza katika majimbo yote. Msimamo wake wa kuwa na sera za kirafiki kwa wakimbzi haukukisaidia - kinyume kabisa. Sio tena chama cha kuongoza maandamano kupinga masuala yanayokwenda kombo. Nafasi hiyo imechukuliwa na chama cha AfD.
Wakati wa uhakika katika siasa za Ujerumani umekwisha. Kila chama kinachotaka kuchukua madaraka ya kuongoza serikali sharti kiwe tayari kwa mazungumzo na vyama vingine. Ujerumani itakuwa na mseto wa vyama vingi kwa sababu wapigaji kura wanataka hivyo. Ni matumaini kwamba vyama vinaelewa ishara hii.
Mwandishi:Fürstenau, Marcel
Tafsiri:Josephat Charo
Mhariri:Mohammed Abdul-rahman