1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni::Ujerumani yajitafakari kufuatia uchaguzi

Ines Pohl | Oumilkheir Hamidou
2 Septemba 2019

Septemba mosi sio tuu ni tarehe ya kihistoria. Mnamo tarehe hiyo hiyo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia - Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD kimejikingia matokeo bora zaidi katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/3OtKb
DW Global Media Forum 2019 | Interview Armin Laschet, Minister President of the German State of North Rhine-Westphalia (NRW), Ines Pohl, Editor in Chief DW Deutsche Welle

Septemba 1, 1939 mnamo saa za alfajiri wajerumani walianzisha vita vikuu vya pili vya dunia kwa kuivamia Poland. Mamilioni waliuwawa, wengine wakajeruhiwa, wanawake wakabakwa, wengine wakatimuliwa na dunia mpaka leo inakabaliwa na makovu ya maangamizi yaliyofanywa na wanazi.

Miaka 80 baadae chama kimoja kinasherehekea ushindi mkubwa nchini Ujerumani, ushindi uliopatikana zaidi kwa kueneza matamshi ya chuki, mtengano na ubaguzi. Katika majimbo ya Saxony na Brandenburg, chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD kimejipatia kote huko matokeo mazuri kabisa. Kwa namna hiyo chama hicho kimefanikiwa katika muda wa miaka michache tu  kugeuka chama cha pili chenye nguvu zaidi katika mabunge ya majimbo hayo. Tusishushe pumzi eti kwasababu zilzala iliyotabiriwa na taasisi za uchunguzi wa maoni ya wapiga kura yaliyoashiria wafuasi hao wa siasa kali za mrengo wa kulia wangepata ushindi mkubwa, haikupiga.

Ujerumani yatanganga

Kipi cha kusema kuhusu nchi hii, Ujerumani ambayo kiuchumi inanawiri na kisiasa ni tulivu, lakini chama kama hicho kinaweza kushinda? Na tutegee kipi pindi majira yakibadilika na Ujerumani pengine kukokotwa na zahma ya misuko suko ya kiuchumi inayoikumba dunia? Kwa kiwango gani tunaweza kujiamini na kusema kamwe chama chenye wafuasi wengi wenye hisia za kibaguzi hakitaruhusiwa kutwaa hatamu za uongozi serikalini?

Walioshindwa ni vyama vyote viwili vikuu, CDU cha Angela Merkel na wana Social Democrat: Wamejipatia matokeo mabaya kabisa kuwahi kushuhudiwa katika majimbo hayo mawili  tangu Ujerumani ilipoungana upya. Mkondo huo unamaanisha kimsingi hali itazidi kuwa ngumu vyama vya jadi vitakapotaka kuunda serikali ya muungano nchini Ujerumani.Yote hayo yanaonyesha jinsi Ujerumani inavyohangaika kujua iwe nchi ya aina gani. Ifuate mkondo wa aina gani katika sera ya wakimbizi na pia katika masuala ya sera ya kiuchumi na jamii. Kipa umbele katika masuala ya kitaifa kiwe cha aina gani na Ulaya ikamate nafasi gani? Kama wahenga wasemavyo watu hujifunza kutokana na yaliyotokea. Kwa namna hiyo yaliyoshuhudiwa Septemba mosi mwaka 2019 tunaweza kuashiria tu kile kitakachoingia katika madaftari ya historia.