1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hannover Messe Auftakt

Charo Josephat21 Aprili 2009

Kansela Merkel ayatembelea maonyesho hayo

https://p.dw.com/p/HanC
Bango la maonyesho ya Hannover mwaka huu lazinduliwaPicha: Deutsche Messe AG

Maonyesho makubwa ya teknolojia yameanza leo mjini Hannover, mji mkuu wa jimbo la Niedersachsen hapa Ujerumani. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameyatembelea maonyesho hayo hii leo ambayo mwaka huu nchi shirika ni Korea Kusini.

Kuanzia leo hadi siku ya Ijumaa waonyeshaji zaidi ya 6,100 kutoka nchi 61 wataonyesha bidhaa zao mpya katika maonyesho ya kimataifa ya teknolojia mjini Hannover. Maonyesho hayo yanaelezwa kuwa makubwa ya bidhaa za viwanda ulimwenguni zilizotengenezwa kutumia teknolojia ya kusimumua.

Kwa miezi kadhaa iliyopita mambo hayajakuwa mazuri sana kwa sekta ya viwanda ya Ujerumani. Hali hii imesababishwa na mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia. Kampuni za Ujerumani katika mwaka mmoja uliopita zimeteteleka kuokoa mikataba na wakati huu ni wateja wachache sana wanaoagiza bidhaa zinazotengenezwa hapa Ujerumani. Mashine zenye chapa, "Made in Germany" ilikuwa vigumu kupatikana mpaka kusuburi kwa muda baada ya kuziagiza. Lakini sasa mambo yamebadilika kwa kasi kubwa.

Juma hili macho yote yanaelekezwa mjini Hannover kwa matumaini kwamba maonyesho hayo makubwa ya bidhaa za viwanda yatasaidia kufufua biashara. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kwa muda wa saa mbili leo amevitembelea vibanda mbalimbali katika maonyesho hayo ya mjini Hannover. Anasema juhudi zinafanywa kuzisaidia kampuni kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi.

"Hatutaki tu kukabiliana na mgogoro wa kiuchumi bali pia tunataka kuyaimarisha makampuni kuondokana na athari za mgogoro huu. Na haya ndiyo mazingira ninayoyahisi mahala hapa. Kampuni za tabaka la kati, kampuni ndogo na hata kampuni kubwa, zinaonyesha bidhaa zao mpya licha ya kuwepo na mazingira magumu ya kiuchumi "

Hannover-Messe 2009 Bundeskanzlerin Angela Merkel, links, und der Ministerpräsident der Republik Südkorea Han Seung Soo eroeffnen am Montag, 20. April 2009, feierlich den koreanischen Stand
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel (kushoto) na waziri mkuu wa Korea Kusini wakitaka utepe kuyafungua maonyesho ya HannoverPicha: AP

Waandaaji wa maonyesho ya mjini Hannover wanasema wamehesabu zaidi ya bidhaa mpya 4,000 zitakazoonyeshwa katika maonyesho hayo. Idadi hii inadhihirisha uwezo mkubwa wa uvumbuzi wa bidhaa uliopo, lakini kwa sasa watumiaji bidhaa wanasitia kununua bidhaa hizo mpya kwa kuwa mabenki yanasita kutoa mikopo. Hali inatarajiwa kuboreka wakati msukosuko wa fedha utakapomalizika. Lakini ni lini msukosuko huo unapotarajiwa kumalizika? Manfred Wittenstein, mfanyabiashara na kiongozi wa chama cha kampuni za kutengeneza mashine anasema,

"Nadhani kwa wakati huu tunaona dalili za hali kuanza kuimarika, lakini hata hivyo hatuna data za kutosha. Tunasubiri kwa mwezi mmoja au miwili ijayo na nafikiri mwanzoni mwa msimu wa kiangazi tutakuwa tumefikia kilele chetu. Na kabla kufikia mwisho wa mwaka huu tutaweza tena kuangalia mbele."

Kauli mbiu ya maonyesho ya Hannover mwaka huu ni utengezaji wa mashine zinazotumia kiwango kidogo cha nishati na nishati mbadala. Katika swala hili Wajerumani wanaongoza ulimwengu na wanataka kuonyesha njia ya kuondokana na tatizo hili.

Licha ya mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia, kuna matumaini makubwa katika maonyesho ya mjini Hannover. Wanaoshiriki katika maonyesho hayo wanaonyesha ukakamavu wa hali ya juu ingawa wanajua haitakuwa rahisi kupata mikataba mipya kutoka kwa wateja wanaotaka kununua bidhaa zao.

Mwandishi: Henrik Böhme/ Charo Josephat

Mhariri: Abdul-Rahman