Maonyesho ya utalii ya nchi za Afrika Mashariki mjini Arusha
11 Oktoba 2021Awali katika uzinduzi wa maonyesho hayo makubwa na ya kwanza kufanyika katika jumuiya hii kongwe barani Afrika, katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki alisisitiza kuwa vikwazo vya kufanya utalii miongoni mwa raia kutoka nchi wanachama viondolewe ili kuweka mazingira rafiki ya kukuza na kutangaza utalii.
Vikwazo kama gharama kubwa katika vivutio vya utalii, vikwazo vya safari katika maeneo ya mipakani na viwanja vya ndege ni miongoni mwa mambo ambayo yamegusiwa.
Rais wa Zanzibar Dr. Husein Mwinyi ameyafunga maonyesho hayo leo, huku akisisitiza kuwa huu unafaa kuwa mwanzo mzuri kwa nchi wanachama kushirikiana kuikuza zaidi sekta ya utalii.
"Tangu mlipuko wa janga la Corona, sekta ya utalii imekumbwa na nyakati mbaya lakini pia kumepatikana fursa ya kuiboresha zaidi na kujifunza mambo mengi. Ninaamini kwamba kupitia maonesho haya makubwa ya kwanza ya utalii ya siku tatu nchi wanachama zimejifunza mambo mengi na kupata fursa za kuikuza biahsara hii.”,alisema Mwinyi.
Soma pia: COVID: Sekta ya utalii duniani kupata hasara ya zaidi ya dola trilioni 4
Kuwekeza katika sekta ya utalii
Maonyesho haya yamehudhuriwa pia na wageni takribani 2000 kutoka nchi mbali mbali duniani na zaidi ya vivutio vya utalii 100 kutoka nchi wanachama za jumuiya ya Afrika Mashariki vimepamba maonyesho hayo. Wadau wa utalii walioshiriki maonyesho hayo wanaona hiyo ni furza nzuri ya kuendelea kuikuza sekta hiyo kwa kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na kuendelea kubadilishana uzoefu.
Soma pia: TANAPA yashinda tuzo kwa utoaji wa huduma za uhifadhi na utalii
Katika maonyesho hayo, hifadhi tano za taifa Tanzania zimetunukiwa tuzo ya ubora wa huduma kwa kiwango cha kimataifa kutoka shirika linalosimamia viwango vya ubora wa bidhaa na huduma nchini TBS.
Hifadhi za Taifa Tanzania Tanapa pamoja na wizara ya maliasili na utalii nchini Tanzania, zinasema kuwa tuzo hiyo imeleta chachu ya kuendelea kutangaza utalii wa Tanzania duniani.