1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Mapambano ya kuwania mji wa Herat yaendelea Afghanistan

31 Julai 2021

Wanajeshi wa Afghanistan na wanamgambo wa Taliban wamepambana tena siku ya Jumamosi kwenye viunga vya pembezoni mwa mji wa magharibi wa Herat.

https://p.dw.com/p/3yMYd
Taliban-Offensive in Afghanistan | Qala-i- Naw
Mapigano yamepamba moto nchini AfghanistanPicha: AFP/Getty Images

Mapambano hayo yametokea siku moja baada ya polisi mmoja kuuwawa wakati majengo ya Umoja wa Mataifa yaliposhambuliwa kwenye mji huo wa magharibi mwa Afghanistan.

Viongozi wa serikali na wakaazi wa mji huo wamearifu kuhusu mapigano hayo mapya ambayo tayari yamesaabisha mamia ya watu kuyahama makaazi yao na kwenda kutafuta hifadhi kwenye maeneo ya katikati mwa mji huo.

Gavana wa mji wa Herat Abdul Saboor Qani amesema mapigano makali zaidi yametokea kwenye wilaya za Injil na Guzara -- kuliko na uwanja wa ndege wa mji huo.

"Hivi sasa mapigano yanaendelea kusini na kusini mashariki. Tunasonga mbele kwa tahadhari na kuepusha vifo vya raia" Gavana Qani amenukuliwa na shirika la habari la AFP.

Mapigano yalikuwa makali pia siku ya Ijumaa

Wakati wa mapigano ya siku ya Ijumaa, majengo yanayotumiwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kutoa msaada kwa Afghanistan kwenye mji wa Herat yalishambuliwa kwa maguruneti na bunduki.

Afghanistan | Bildergalerie | Truppenabzug
Picha: HOSHANG HASHIMI/AFP/Getty Images

Umoja wa Mataifa umesema shambulizi hilo lilifanywa na watu wanaoipinga serikali.

Wapiganaji wa Taliban wamesema mara kadhaa hawatawalenga wanadiplomasia wa kigeni wanaolindwa na sheria za kimataifa lakini wamekiuka ahadi hiyo mara kadhaa.

Machafuko bado yametapakaa nchini Afghanistan

Duru zinaarifu jeshi la Afghanistan kwa kushirikiana na mbabe wa kivita anayelipinga kundi la Taliban Ismail Khan wamepeleka wapiganaji kadhaa kuwania mji huo wa wakaazi 600,000.     

Afghanistan | Konfliktregion in Nahost
Picha: Reza Shirmohammadi/AFP/ Getty Images

Khan, ambayo alipigana vita dhidi ya uvamizi wa uliokuwa Muungano wa Kisovieti katika miaka ya 1980 na baada dhidi ya kundi la Taliban miaka ya 1990 ameapa kupigana na waasi hao kwa mara nyingine ambao wamekuwa wakipata mafanikio siku za karibuni.

Machafuko yametapakaa kote nchini Afghanistan tangu mapema mwa mwezi Mei pindi kundi la Taliban lilipoanzisha mashambulizi makali na mapana wakati vikosi vya majeshi ya kigeni vilivyokuwa vikiongozwa na Marekani vilipoanza hatua ya mwisho ya kuondoka kikamilifu nchini humo.

Wanamgambo hao wameyakamata maeneo kadhaa makubwa nchini Afghanistan ikiwemo wilaya kwenye jimbo la Herat, ambako kundi hilo limechukua udhibiti wa vituo viwili vya mipaka kati ya Afghanistan na mataifa jirani ya Iran na Turkmenistan.