1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano Gaza

11 Januari 2009

Katika siku ya 16 ya mapigano Gaza,raia 6 wa kipalestina wauwawa.

https://p.dw.com/p/GW2c
Wanajeshi wa IsraelPicha: picture-alliance/ dpa

Shirika la habari la Ufaransa AFP, linaarifu kwamba raia 6 wa kipalestina pamoja nao watoto 4 wameuwawa leo katika hujuma ya majeshi ya Israel huko kaskazini mwa mwambao wa Gaza.

Nae waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amesema leo kwamba Israel inakaribia kuzifikia shabaha zake ilizojiwekea katika vita hivi huko Gaza lakini itaendelea na hujuma za kupambana na Hamas kwa hivi sasa.

Hapo kabla, Israel ilidondosha kutoka hewani vipeperushi vikiwaonya wakaazi milioni 1.5 wa mwambao wa Gaza kwamba karibuni yamkini ikaimarisha hujuma zake dhidi ya wapiganaji wa Hamas.Inapanga kuhujumu mahandaki yanayotumika kuingiza silaha Gaza kimagendo pamoja na ghala za silaha za chama cha Hamas.

Hamas kwa upande wake, imepewa nasaha na Rais Mahamud Abbas wa Palestina kuuridhia mpango wa amani wa Misri.Kiongozi wa Hamas anaeishi uhamishoni,Khaled Meshaal amesema mjini Damascus,Syria, kwamba mapatano yoyote ya kusimamisha vita lazima yatanguliwe na Israel kusimamisha hujuma zake kwanza.Taarifa yake hiyo imekuja wakati hujuma za anga na za ardhini za majeshi ya Israel zikiingia siku yake ya 16.

Watumishi wa hospitali wanaohudumia majeruhi huko Gaza wanaarifu kwamba idadi ya wapalestina waliouwawa sasa imefikia 850.Katika idadi hiyo, Israel inadai mamia ni wapiganaji wa Hamas.Mnamo wiki 2 za mapigano,Israel imepoteza wanajeshi wake 10 na raia 3 waliouwawa.