Mapigano yaendelea Msumbiji
31 Machi 2021Wakati mapambano kati ya vikosi vya serikali na waasi yakipindukia wiki nzima sasa, mashirika ya Umoja wa Mataifa yana wasiwasi kwamba wanawake na watoto wamekuwa wakilengwa kwa makusudi ambapo maelfu wanayakimbia makaazi yao.
Yakitowa kile wanachosema ni "indhari ya hali mbaya ya kibinaadamu" hapo jana (Machi 30), mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yameripoti kwamba watu wamekuwa wakiuawa na waasi ambao hawakusema ni wa makundi gani.
Katika mji wa kaskazini wa Palma ulio jimbo la Cabo Delgado, vifo na majeruhi kadhaa wameripotiwa.
"Kinachotokezea Palma kwa hakika ni balaa kubwa sana linalofanywa na kundi lenye silaha dhidi ya raia. Wamefanya mambo ya kutisha na bado wanaendelea. Hata asubuhi ya leo tuna ripoti za kutokea mapigano makali. Ndiyo maana tunazungumzia hofu zetu kwamba maelfu ya watu wanakimbia wilaya ya Palma kuelekea maeneo mengine ya nchi na kuelekea mpaka wa Tanzania." Alisema Jens Laerke, msemaji wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), ambaye pia alithibitisha kwamba kwa zaidi ya wiki moja sasa, mapigano yanaendelea bila kusita.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji (IOM) lilisema kwamba hali ni mbaya kwa watu wanaokimbia mapigano hayo, hasa kwa wanawake na watoto ambao wanalazimika kulala misituni.
Kufikia asubuhi ya Jumanne, watu 3,361 kutoka familia 672 walishasajiliwa na IOM kuwa wakimbizi wa ndani, kwa mujibu wa msemaji wa shirika hilo, Paul Dillon, ambaye alisema watu hao wanawasili kwa miguu, mabasi, ndege na boti kutoka mji wa Palma kwenda miji ya Ulongwe, Mueda, Montepuez na Pemba.
Vifo na wakimbizi Cabo Delgado
Tangu mzozo huo uanze mwezi Oktoba 2017, watu 670,000 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao, zaidi ya nusu wakiwa watoto wadodo, kwa mujibu wa msemaji wa Shirika la Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Marixie Mercado.
Mapigano ya awamu hii yalianza siku ya Jumatano baada ya waasi wapatao 100 kuuvamia mji wenye utajiri wa gesi wa Palma.
Mkurugenzi wa kampuni ya masuala ya ulinzi ya DAG, Max Dyck, aliliambia shirika la habari la Ujerumani (dpa) kwamba inaonesha waasi wamejipanga vyema zaidi, na wafanyakazi wa kampuni yake wamekuwa wakijaribu kuwafikia na kuwaokowa mamia ya watu, lakini mara kadhaa wanajikuta wakishambuliwa.
Kundi lijiitalo Dola la Kiislamu lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, linasema limechukuwa udhibiti wa mji wa Palma na limewauwa zaidi ya wanajeshi 55 wa Msumbiji.
Kampuni ya mafuta ya Ufaransa, Total, imewahamisha wafanyakazi wake wapatao 1,000 kutoka kwenye mkoa huo ambako imewekeza dola bilioni 20 kwenye mradi wa uchimbaji gesi asilia.
Kwa mwaka wa tatu sasa, mkoa wa huo Cabo Delgado wenye utajiri mkubwa wa mafuta umeshuhudia mashambulizi ya mara kwa mara ambayo yamepoteza maisha ya watu 2,500.