Mapigano kati ya jeshi la kundi la RSF yaendelea Sudan
15 Aprili 2023Kikosi maalumu cha wanamgambo cha Rapid Support Forces, RSF cha nchini Sudan kimedai kuwa kinadhibiti ikulu ya rais, makao makuu ya jeshi na uwanja wa ndege wa mji mkuu, Khartoum, katika kile kinachoonekana wazi kuwa jaribio la mapinduzi.
Hata hivyo, jeshi la nchi hiyo limesema linapambana na RSF katika vituo inavyodai kuvidhibiti, zikiwemo kambi mbili za jeshi za Merowe na el-Obeid.
Milio ya silaha nzito nzito imesikika katika maeneo mengi ya Sudan, ambapo kikosi cha RSF kimesema kilijitetea baada ya kushambuliwa kwanza na jeshi.
Saudi Arabia imefuta safari za ndege zake kutoka na kuingia Sudan, baada ya kusema kuwa ndege yake moja imekumbwa na mkasa kwenye uwanja wa Khartoum.
Mataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Urusi, na Umoja wa Mataifa yamezitaka pande zinazohasimiana nchini Sudan kuacha mapigano mara moja.
Chanzo: RTRE