Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF bado kizungumkuti
5 Julai 2023Mzozo kati ya jeshi la serikali ya Sudan na kikosi cha msaada wa dharura cha RSF bado unaendelea kuididimiza nchi hiyo ambayo kwa zaidi ya miezi miwili bado inakabiliwa na vita vya makundi hayo mawili yanayowania madaraka.
Soma zaidi:Mji wa Khartoum watikiswa na miripuko kwa mara nyingine
Kikosi cha RSF kinatajwa kuchukua udhibiti wa maeneo makubwa ya mji mkuu wa Khartoum huku duru zikiarifu kuwa jeshi hilo sasa limeongeza wapiganaaji wa ziada kutoka Darfur na Kordofan ambao wanasambazwa katika miji ya Omdurman , Bahri na Khartoum, miji mingine yenye makutano ya mto Nile ili kuongeza udhibiti wao.
Mashuhuda wa mapigano yaliyotokea jana huko wanasimulia kwamba mapigano hayo yalikuwa ni makali na kwamba jeshi la serikali lilikuwa likijaribu kuzuia kikosi cha RSF ambacho kilihitaji kukitwaaa moja ya kituo cha polisi.
Soma zaidi: Mapigano makali kati ya vikosi vya majenerali wanaohasimiana yautikisa mji wa Khartoum nchini Sudan
Mzozo huo uliibuka katikati mwa mabishano kuhusu mpango unaoungwa mkono na jumuiya ya kimataifa wa kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia, miaka minne tangu kupinduliwa kwa aliyekuwa mtawala wa muda mrefu Omar al-Bashir.
Kwa upande mwingine Mapigano makali pia yameripotiwa kutokea katika eneo zima la mji mkuu wa Sudan ambako mashahidi wameeleza juu ya kuangushwa kwa ndege moja ya kivita, huku mashambulio ya makombora na bunduki yakiyatikisa maeneo mengi yanayouzunguka mji huo.
Chanzo kutoka kikosi cha wanamgambo cha RSF kimeeleza kwamba kundi hilo limehusika kuidungua ndege hiyo ya jeshi la serikali ya Sudan na Kikosi cha RSF kimesema kimemkamata rubani baada ya kutuwa kwa mwavuli.
Wakati mapigano makali yakiendelea kushuhudiwa hasa katika mji mkuu wa Khartoum na eneo la magharibi la Darfur, mamia ya raia walionaswa katika maeneo hayo wanatajwa kukosa huduma muhimu za kijamii ikiwemo maji, chakula, dawa kwa karibu miezi mitatu sasa .
Kwa mujibu wa shirika lakimataifa la uhamiaji , hadi sasa takriban Wasudan milioni 2.2 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi na zaidi ya watu laki sita wakivuka mipaka kutafuta sehemu zenye usalama.