1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMsumbiji

Machafuko Msumbiji yasababisha maelfu kuyakimbia makaazi yao

22 Februari 2024

Takwimu zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinasema wimbi jipya la machafuko yatokanayona uasi Kaskazini mwa Msumbiji, yamesababisha maelfu ya watu kukimbia makaazi yao katika mkoa wa Cabo Delgado.

https://p.dw.com/p/4ckd7
Mosambik Cabo Delgado | Flüchtlinge in Cabo Delgado nach Terror Angriff in Palma
Baadhi ya raia waliolikimbia eneo la Cabo Delgado kufuatia machafuko mapya ya makundi ya wanamgambo walio na itikadi kali Picha: DW

Tahadhari iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia uhamiaji IOM imesema mashambulizi ya hivi karibuni katika mikoa ya Macomia, Chiure na Mecufi yamesababisha watu 13,088 kupoteza makaazi yao. Wengi wa waliokuwa wanatoroka maeneo hayo ya machafuko ni watoto waliotumia mabasi, maboti na hata wengine kutembea kwa miguu, kukimbilia mahali salama.

Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi amethibitisha kwamba kumekuwepo na wimbi jipya la watu wanaoitoroka nchi, hakukizungumzia kitisho kilichopo lakini alisisitiza kwamba maafisa wa usalama wameidhibiti hali hiyo. Nyusi amesema watu walioonekana kuutoroka mji wa Ocua hivi karibuni walikuwa wanayakimbia mashambulizi ya kulipiziana kisasi baada ya wanajeshi wa Msumbiji na Rwanda kufanikiwa kuvunja jaribio la utekaji nyara wa watoto katika eneo hilo.

Kulingana na msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia wakimbizi UNHCR  mwezi uliopita kulikuwa na idadi ya makundi ya wanamgambo waliojihami Kusini mwa mji wa Cabo Delgado. Ameongeza kuwa mashambulizi yaliyofanywa huko yaliharibu vibaya makanisa, nyumba za watu, shule, miundo mbinu na hata taasisi za afya.

Licha ya wanajeshi wa SADC kuwepo bado uasi unaendelea kwa kasi kubwa

Mosambik Nationale Verteidigungsstreitkräfte Südafrikas (SANDF)
Wanajeshi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC wameisadia Msumbiji kuyatwaa tena maeneo yaliyokuwa yametekwa na makundi ya wanamgambo.Picha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Tobias Miguel, mtafiti anaefuatilia hali ya machafuko nchini humo amesema wale wanaoitoroka nchi wanakimbilia Kaskazini mwa mji wa Pemba au kuingia katika mkoa jirani wa Nampula. Waziri wa mkoa huo Jaime Neto, amesema tasisi ya kitaifa ya kushughulikia majanga inapanga kufungua shirika la kuwahifadhi watu hao waliopotezuka makaazi yao.

Wanajeshi kutoka Rwanda na wale wa kutoka mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC walipelekwa Msumbiji mwezi Julai mwaka 2021 baada ya miaka kadhaa ya uasi kutoka kwa makundi ya wanamgambo walio na itikadi kali.

Wanajeshi hao wameisadia nchi hiyo kuyatwaa tena maeneo yaliyokuwa yametekwa huko Cabo Delgado lakini licha ya hayo bado vurugu za mara kwa mara zinashuhudiwa. Mfanyakazi mmoja wa Umma katika eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe amethibitisha kuwa hali inazidi kuwa mbaya na kwamba makundi hayo yaliyojihami yamerejea tena na kushambulia kwa nguvu kali zaidi.

Jeshi la Msumbiji ladhibiti mji wa Mocimboa da Praia

afp