1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano mapya Sudan Kusini

Jane Nyingi
17 Oktoba 2016

Majeshi ya Sudani Kusini yamewashtumu waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais,Riek Machar, kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya kuyashambulia maeneo yao yaliyo karibu na Mto Nile,

https://p.dw.com/p/2RJXw
Konflikt im Südsudan Regierungssoldaten 19.12.2013
Majeshi ya serikali yakipuga doria mjini JubaPicha: picture-alliance/dpa

Zaidi ya watu 50 wanaripotiwa kuuawa kufuatia mapigano hayo nje ya mji wa Malakal, mwishoni mwa wiki. Msemaji wa jeshi nchini humo Brigedia Lul Ruai Koang amesema majeshi ya Machar yakiongozwa na Jenerali Johnson Olony yalishambulia maeneo ya Warjuak na Leleo karibu kilomita 20 kaskazini mwa mji wa Malakal. Karibu wanajeshi 50 wanaomuunga mkono Machar waliuawa huku upande wa serikali inayoongozwa na rais Kiir ikiwapoteza wanajeshi sita.

Msemaji huyo amewahakikishia wakaazi wa South Sudan kuwa wanajeshi hao wa Machar hawakufanikiwa kuuteka mji wa Malakal kama iliyoripotiwa awali. "Mwisho wa yote Riek Machar atawajibishwa, kwa mfano mashambulizi dhidi ya raia katika eneo la Jalhak na Rome ambapo wapiganaji wake walikuwa wakipokea agizo kutoka kwa generali Olony.Hayo ni mambo yaliyowazi, sawa na jimbo lilo kusini la Liech, makamanda wa eneo hilo wanafahamika. Iwapo hautataweza kumchukulia hatua jamii ya kimataifa itahakikisha Riek Machar anafikishwa mahakamani" alisema Brigedia Koang

Mashambulizi zaidi yatazamiwa

Brigadier Lul Ruai Koang amesema wanatazamia mashambulizi mengine kutoka upande wa Machar. Pande zote mbili zilikubaliana kusitisha mapigano mwezi Julai mwaka huu baada ya kuzuka upya vita vilivyosababisha vifo vya karibu watu 300. Mwezi Aprili rais Salva Kiira na Machar waliunda serikali ya umoja wa kitaifa iliyolenga kumaliza mauji ya kikatili yaliyoendelea kwa karibu miaka mitatu kutokana na vita.

Südsudan Waffenstillstand 01.02.2014 Addis Abeba
Rais Salva Kiir (Kushoto) Makamu wa zamani wa rais Riek Machar(Kulia)Picha: Reuters/T. Negeri

Hata hivyo mapigano yaliyozuka upya mwezi Julai yalivuruga juhudi za amani baada ya Machar kuondoka nchini humo na kuingia Kongo kupitia eneo la mpakani. Kwa sasa makamu huyo wa zamani wa rais wa Sudan Kusini anapatiwa matibabu nchini Afrika Kusini. Katika mahojiano ya kipekee na DW Machar ameishtumu serikali ya rais Kiir kwa kutokuwa makini kupata ufumbuzi wa kusitishwa mapigano ambayo yameendelea kwa muda mrefu nchini Sudan Kusini. Karibu watu million 2.5 wameyakimbia makaazi yao katika kipindi cha miaka miwili ya mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha mauaji, ubakaji wa magenge na watoto kusajiliwa kwa lazima jeshini.

Südsudan Kindsoldaten
Watoto waliosajiliwa jeshiniPicha: picture-alliance/dpa/AA/S. Bol

Raia laki mbili wamepewa hifadhi ndani ya kambi za Umoja wa Umoja wa mataifa nchini humo. Jamii ya kimataifa imelaumiwa kwa kukosa kufanikisha makubaliano ya mwaka 2015 ambayo yamesababisha hali inayoendelea kwa sasa nchini Sudan Kusini. Wiki iliyopita karibu watu 60 waliuawa na Umoja wa Mataifa unasema ulipokea ripoti ya kuchomwa moto baadhi yao wakiwa hai ndani ya mabasi.

Mwandishi: Jane Nyingi/afp/rtre/interview Africalink

Mhariri: Mohammed Khelef