1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano mapya yazuka Sudan Kusini

17 Desemba 2013

Milio mipya ya risasi imesikika kwenye mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba mapema leo asubuhi, siku moja baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kutangaza kuwa amefanikiwa kuzima jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali yake.

https://p.dw.com/p/1Aaqo
Kifaru cha kijeshi kikifanya doria mjini Juba
Kifaru cha kijeshi kikifanya doria mjini JubaPicha: Reuters

Milio ya risasi ikiwemo ile ya silaha za kivita, imesikika tena majira ya leo asubuhi kutokea kwenye makao makuu ya jeshi, kilomita chache kutoka katikati ya mji mkuu, Juba. Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamin amesema kuwa mapigano mapya yalianza tena usiku wa kuamkia leo.

Amesema kuwa jeshi limewakamata viongozi watano wa kisiasa wanaotuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi ambalo limeshindwa.

Rais Salva Kiir wa Sudan
Rais Salva Kiir wa SudanPicha: Reuters

Amesema jeshi hilo linaendelea kuwatafuta watu wengine zaidi wanaotuhumiwa kuhusika.

Watu waliondolewa katika mitaa ya mji huo, huku magari ya kijeshi tu ndiyo yakionekana na raia wakijifungia majumbani mwao. Jana Rais Kiir alisema kuwa nchi hiyo iko salama baada ya kutokea jaribio hilo la mapinduzi na hali ya usalama imedhibitiwa.

Kiasi watu 26 wameuawa

Wakati huo huo, Waziri wa masuala ya baraza la mawaziri, Martin Elia Lomuro, amesema kuwa kiasi watu 26 wameuawa katika mapigano yaliyoanza siku ya Jumapili muda mfupi kabla ya usiku wa manane.

Waziri Lomuro ameongeza kusema kuwa wengi wa waliouawa ni wanajeshi. Vituo vya redio vya Sudan Kusini vimeripoti kuwa watu wapatao 130 wamejeruhiwa na wamelazwa hospitalini.

Rais Kiir amewalaumu wanajeshi watiifu kwa makamu wake wa zamani, Riek Machar aliyefukuzwa kazi mwezi Julai mwaka huu, kwa kuanzisha mapigano na kupanga jaribio la mapinduzi kwa lengo la kuiangusha serikali iliyoko madarakani.

Makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini, Riek Machar
Makamu wa rais wa zamani wa Sudan Kusini, Riek MacharPicha: Stan Honda/AFP/Getty Images

Machar analiongoza kundi la upinzani ndani ya chama cha Sudan People's Liberation Movement-SPLM na kundi hilo linaonekana kuwa lenye upinzani mkubwa kwa Rais Kiir.

Mahasimu hao wawili wanatokea katika makabila mawili tofauti na wamekuwa wakipigana katika pande tofauti wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.

Marekani yaifatilia hali ya kiusalama

Ama kwa upande mwingine Marekani imesema inaifuatilia kwa karibu hali ya kiusalama nchini Sudan Kusini baada ya kuzuka kwa mapigano.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani, Marie Harf, amesema kuwa Marekani imezitolea wito pande zote kutatua tofauti zao kupitia njia za amani za kidiplomasia na sio kwa njia ya mapigano.

Rais wa Marekani, Barack Obama
Rais wa Marekani, Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Harf amesema hali nchini Sudan Kusini siyo nzuri na hivyo Marekani itaendelea kuifatilia kwa karibu nchi hiyo kwa sababu wasiwasi wake mkubwa ni usalama wa raia wa Marekani walioko nchi za nje.

Sudan Kusini ilijipatia uhuru wake mwaka 2011 baada ya wananchi wake kupiga kura ya maoni ya kujitenga na Sudan na kuanzisha taifa hilo jipya. Nchi hiyo ina utajiri mkubwa wa mafuta lakini bado wananchi wake wanaishi katika umaskini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Gakuba Daniel