1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yachacha nchini Pakistan

Charo Josephat8 Mei 2009

Wanamgambo 12 wauwawa katika bonde la Swat

https://p.dw.com/p/Hlzr
Mwanajeshi wa Pakistan akishika doria katika eneo la Dir linalopakana na bonde la SwatPicha: picture-alliance/ dpa

Ndege za jeshi la Pakistan zimezishambulia ngome za wanamgambo wa Taliban katika jimbo la Swat hii leo, siku moja baada ya waziri mkuu wa nchi hiyo kuliamuru jeshi kuwachakaza magaidi na Marekani kuahidi kuisadia Pakistan kupambana na wanamgambo wa Taliban na Al Qaeda. Wakati huo huo, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema watu nusu milioni wamekimbia kutoka kaskazini magahribi mwa Pakistan katika siku chache zilizopita.

Wanajeshi wa Pakistan wakisaidiwa na helikopta za kivita wamekabiliana na wanagambo katika bonde la Swat ambapo wapiganaji 12 wameuwawa. Msemaji wa jeshiu la Pakistan, meja Nasir Khan, amesema mauaji ya wanamgambo hao yanafuatia kuuwawa kwa wanamgambo wengine 55 hapo jana.

Lakini huku helikopta zikiendelea kuzishambuli ngome za wanagambo, wanajeshi wa nchi kavu wamekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanamgambo, wengi wao wakiwa ni vijana wenye itikadi kali ya kidini na wanaolipwa mishahara minono.

Waziri mkuu wa Pakistan Yusuf Raza Gilani alitangaza jana katika hotuba yake ilioonyeshwa kwenye televisheni kwamba wanamgambo wa Taliban wanajaribu kuishika mateka Pakistan kwa kuielekezea mtutu wa bunduki na kuanzisha harakati kubwa ya kijeshi dhidi ya wanamgambo hao katika bonde la Swat, ambako mkataba wa amani umesambaratika.

Waziri mkuu Yusuf Raza Gilani ametoa mwito Wapikistan waungane katika vita dhidi ya wanamgambo wenye siasa kali ambao amesema wanatishia uhuru wa taifa na ambao wamekiuka mkataba waliokubaliana na serikali ya mjini Islamabad.

Ndege za kivita zimeanza tena mashambulio katika maeneo yanayoshukiwa kuwa ngome za waasi katika miji ya Matta, Kabal na Khazakhela katika wilaya ya Swat kufuatia usiku wa mapambano makali katika eneo hilo lililo na idadi kubwa ya wapiganaji wa Taliban.

Afisa mmoja katika eneo hilo amesema vikosi vya serikali vinasonga mbele kuelea eneo la chini la Dir na usiku wa jana kulikuwa na mashambulio mengi ya mabomu katika mji wa Miadan katika siku 12 zilizopita. Afisa huyo hata hivyo hakuweza kuthibitisha idadi ya watu waliouwawa au kujeruhiwa kutokana na opresheni inayoendelea katika eneo hilo.

Wakaazi wanasema huku wanajeshi wakisonga mbele kuelekea eneo la kaskazini la Pakistan, mawasiliano ya simu yamekatika katika eneo hilo na hakuna anayeweza kuwasiliana na mtu yeyote aliye nje ya eneo hilo.

Flucht aus dem Swat-Tal
Wakaazi wa bonde la Swat wakiyakimbia makazi yaoPicha: AP

Wakazi wakimbia mapigano

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi, UNHCR, linasema watu nusu milioni wameyakimbia mapigano kaskazini magharibi mwa Pakistan katika siku chache zilizopita. Idadi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na machafuko nchini Paklistan katika miezi ya hivi karibuni sasa imefikia milioni moja.

Ron Redmond, msemaji wa kamishna wa mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia maswala ya wakimbizi anasema mapigano yamesababisha idadi kubwa ya watu kuachwa bila makazi katika maeneo ya vita kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva nchini Uswisi hii leo, msemaji huyo aidha amesema takriban watu 200,000 wamewasili katika maeneo yaliyo salama katika siku chache zilizopita na wengine 300,000 wamo njiani kukimbia mapigano au wanajiandaa kuanza safari ya kuondoka makwao kwenda kwenye sehemu zilizo salama.

Mwandishi: Josephat Charo/RTRE

Mhariri: Othman Miraji