1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yanaendelea nchini Libya

Abdu Said Mtullya6 Machi 2011

Mapigano bado yanaendelea nchini Libya na waasi warudi nyuma katika mji wa Ras Lanuf

https://p.dw.com/p/10UCR
Kiongozi wa Libya Kanali Gaddafi.Picha: AP

Majeshi yanayomtii Kanali Gaddafi yamewashambulia waasi katika mji wa Bin Jawad uliopo kati ya mji wa Sirte na wa Ras Lanus unaodhibitiwa na wapinzani wa Gaddafi.Waasi wametoa taarifa hiyo leo.

Mpiganaji mmoja wa waasi alierejea kutoka kwenye uwanja wa mapambano akiwa amejeruhiwa amesema majeshi ya Gaddafi yanafanya mashambulio kwa kutumia bunduki za rashasha na magurunedi yanayorushwa kwa roketi.Mpiganaji huyo amesema alichokiona ni vifo tu.

Waasi wengine katika mji wa Ras Lanuf wamesema kuwa wamepata taarifa ya mashambulio ya majeshi ya Gaddafi kwa njia ya simu kutokea kwenye uwanja wa mapambano.Waasi wameambiwa na watu kwamba majeshi ya Gaddafi yapo katika mji wa Bin Jawad.

Wakati huo huo wakaazi wa mji wa Misrata wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba mji huo bado umo katika mikono ya wapinzani wa Gaddafi. Mji huo upo umbali wa kilometa 200 mashariki ya mji mkuu, Tripoli.

Taarifa hizo zinakanusha habari zilizotangazwa na televesheni ya serikali kwamba majeshi ya Gaddafi yameuteka tena mji huo. Mkaazi mmoja wa mji huo ambae hakutaka kutajwa jina ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba mji huo sasa upo katika hali shwari.Hata hivyo mtu huyo amesema alisikia milio ya silaha karibu na uwanja wa ndege leo asubuhi.