Maporomoko ya ardhi yaua watu 10, DRC
10 Mei 2023Matangazo
Hayo yamethibitishwa leo na maafisa katika eneo ambalo mamia ya watu walifariki wiki iliyopita kufuatia mafuriko makubwa. Kiongozi wa eneo la Lubero, la mkoa wa Kivu Kaskazini Edgard Kasombolene amesema maporomoko hayo ya ardhi yalitokea jana usiku katika kijiji cha Miringati. Kamanda wa polisi wa Lubero Kanali Jean Habamungu amesema shughuli ya kuwatafuta walionusurika inaendelea. Mkasa huo wa karibuni unafuatia mvua kubwa iliyonyesha na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi yaliyoathiri mashariki mwa Kongo katika siku za karibuni. Zaidi ya watu 400 walikufa wiki iliyopita katika mkoa wa Kivu Kusini baada ya mafuriko makubwa kulikumba eneo la Kalehe la mkoa huo.