Marais Joe Biden na Xi Jinping wazungumza kuhusu Ukraine
18 Machi 2022Mazungumzo baina ya viongozi hao ni sehemu ya juhudi za kidiplomasia kuhusu mzozo huo, ambazo zimehusisha nchi kadhaa katika mabara tofauti.
Afisa mkuu wa habari katika Ikulu ya mjini Washington, Jen Psaki amesema mazungumzo baina ya marais Biden na Xi yameanza saa tisa alasiri majira ya Afrika Mashariki, na kuongeza kuwa yatakuwa kipimo cha msimamo wa China juu ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.
Wakati afisa huyo wa Marekani akisema Biden atambana Xi kuhusu matamshi ya China yanayoshindwa kuikemea hatua ya Urusi, China yenyewe imeikosoa Marekani, ikisema inaichokoza Urusi na kuchochea moto wa vita, kwa kuipelekea Ukraine shehena za silaha.
China katika juhudi za kuupa nguvu mtazamo wake
Katika kile kinachochukuliwa kama kuupigia debe msimamo wa China juu ya vita vya nchini Ukraine, msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo amesema kuwa kabla ya mazungumzo na Biden, Xi Jinping alizungumza na rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa na wa Cambodia Hun Sen, na kwamba mitazamo ya marais hao ilikubaliana na China.
Soma zaidi: UN: Zaidi ya raia 700 wameuawa nchini Ukraine
Taarifa za awali kutoka mazungumzo baina ya Biden na Xi, ambazo zimechapishwa na shirika la habari la China, zimesema kuwa Rais Xi Jinping amemuambia Joe Biden mzozo wa Ukraine ni kitu ambacho China isingependa kukiona, na kuongeza kuwa mahusiano baina ya nchi na nchi hayawezi kujengwa kwenye msingi wa mivutano.
Kansela wa Ujerumani ahimiza kumalizika kwa vita
Mapema leo, Kansela wa Ujerumana Olaf Scholz amempigia simu rais wa Urusi Vladimir Putin, na kuhimiza kufikiwa haraka kwa makubaliano ya kumaliza vita baina ya Urusi na Ukraine.
Tangazo la Ikulu ya Urusi baada ya mazungumzo ya viongozi hao, limesema Putin amelalamikia mauaji ya raia aliyosema yanafanywa na vikosi vya Ukraine katika miji ya mashariki mwa nchi hiyo, akisema nchi za magharibi zinavifumbia macho vitendo hivyo vya Ukraine.
Soma zaidi: Wanajeshi 70 wa Ukraine wauwawa
Katika masuala mengine ya kidiplomasia, Bulgaria imeamuru kufukuzwa kwa wafanyakazi 10 wa ubalozi wa Urusi nchini humo, ikisema wamekiuka mipaka ya kazi zao. Vile vile nchi tatu za ukanda wa Baltiki, Lithuania, Estonia na Latvia pia zimewatimua wanadiplomasia wengine 10 wa Urusi, sambamba na upinzani wa nchi hizo dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Urusi imesema itajibu kwa hatua sawa na hizo.
Matatizo ya kibinadamu yatokanayo na vita vya nchini Ukraine nayo yamekuwa yakiongezeka, ambapo leo hii imearifiwa kuwa tayari wakimbizi miliyoni mbili kutoka Ukraine wamekwishaingia nchini Poland pekee. Umoja wa mataifa umesema raia 780, wakiwemo watoto 58 wamekwishauawa nchini Ukraine tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi siku 23 zilizopita.
ape, rtre