1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais wa jumuiya ya SADC waidhinisha kupelekwa jeshi Kongo

Saleh Mwanamilongo
18 Agosti 2023

Marais wa Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya kusini mwa Afrika, SADC, wameridhia kupelekwa kikosi cha kulinda amani mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/4VJir
 Jumuiya ya SADC yaridhia kupelekwa kikosi cha kulinda amani mashariki mwa Kongo
Jumuiya ya SADC yaridhia kupelekwa kikosi cha kulinda amani mashariki mwa KongoPicha: DW

Kwenye mkutano huo wa Luanda, Angola , Marais wa Jumuiya ya SADC walipewa taarifa kuhusu hali ya usalama mashariki mwa Kongo na kuidhinisha kutumwa kwa wanajeshi wa nchi za SADC huko jimboni Kivu.

Taarifa ya pamoja ya mkutao huo imesema marais wa jumuiya ya SADC wamesisitiza wito wao wa kuimarisha uratibu na uwianishaji wa mipango ya amani mashariki mwa Kogo baina ya pande inne husika ikiwemo jumuiya ya Afrika Mashariki, jumuiya ya nchi za Afrika ya Kati na Kongomano la nchi za Maziwa Makuu ICGLR. Marais hao wa jumuiya ya SADC wamempongeza pia rais wa Angola, Joao Lourencou, katika juhudi zake za upatanishi baina ya Kongo na Rwanda ili kutatua mzozo wao kwa jia ya amani.

Kikosi cha SADC kuundwa na nani ?

Hata hivyo haija bainika wazi ni lini na nchi zipi zitatuma wanajeshi wake huko mashariki mwa Kongo. Mwezi Machi , Angola ilitangaza kuchangia wanajeshi mia tano katika kikosi hicho cha SADC mashariki mwa Kongo, lakini ilifahamisha kwamba wanajeshi hao watahusika tu na kusimamia mchakato wa kuwapokonya silaha wapiganaji wa M23.

Namibia pia ilionyesha utayari wake wa kuwapeleka wanajeshi wake huko Kongo. lakini kwenye mkutano wa hapo jana hakukuweko na hatua zaidi katika kukamilisha mchakato huo. Mwezi Mei, Rais wa Kongo, Felix Tshisekedi alitishia kuwaondoa wanajeshi wa Afrika mashariki endapo hakutokuweko na mafanikio yoyote huko Kivu katika kuyasaka makundi ya waasi likiwemo lile la M23.

''Wasipoondoka tutawamaliza ''

Mnamo Novemba 2021, Uganda ilituma wanajeshi kusaidia wanajeshi wa Kongo kuwasaka waasi wa ADF katika ya operesheni ya pamoja
Mnamo Novemba 2021, Uganda ilituma wanajeshi kusaidia wanajeshi wa Kongo kuwasaka waasi wa ADF katika ya operesheni ya pamojaPicha: Alain Uaykani/Xinhua/picture alliance

Wakati huohuo, majeshi ya Uganda na Kongo ambayo yanapambana na kundi la waasi wa ADF huko Kivu na Ituri yanasema yaliwaua zaidi ya waasi 548 mnamo kipindi cha miaka miwili ya operesheni ya pamoja. Akizuru eneo la Mwalika huko Beni, mkuu wa jeshi la ardhini la Uganda, Lt jenerali Kahanja Muhanga amesema wamepunguza uwezo wa waasi wa ADF.

''Tunakuja sasa hapa Mwalika, na hapa lazima waasi wa ADF waondolewe. Wasipo ondoka tutawamaliza. Nimekutaa na makamanda wa majeshi ya UPDF ( Uganda) na FARDC ( Kongo) ilikuendeleza operesheni zetu.'', alisema Kahanja.

Kwa upande wake msemaji wa opereshe hiyo ya pamoja ya jeshi la Kongo na Uganda, ameiambia DW kwamba waasi wengine 50 wamekamatwa, 31 wamejisalimisha na raia zaidi ya 156 wameokolewa kutoka kwa waasi hao mnamo kipindi cha operesheni hiyo.