1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marais wa Urusi na Iran wasaini makubaliano ya ushirikiano

17 Januari 2025

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin wamesaini ''mkataba wa ushirikano wa kina wa kimkakati'' katika hatua ambayo huenda ikasababisha wasiwasi kwa serikali za Magharibi.

https://p.dw.com/p/4pISl
Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian
Rais wa Urusi, Vladimir Putin na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian Picha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Viongozi hao wawili wamekutana Ijumaa kwenye Ikulu ya Urusi, Kremlin mjini Moscow, ambapo wamejadiliana kuhusu uhusiano baina ya nchi hizo mbili na wamesaini mkataba wa kuimarisha uhusiano wa kijeshi na kiuchumi, ambao Rais Putin ameuita wenye mafanikio.

Rais Pezeshkian ambaye anaizuru Urusi kwa mara ya kwanza tangu alipoingia madarakani, amesema makubaliano hayo yataimarisha ''msingi thabiti wa harakati zao kusonga mbele.'' Aidha, amebainisha kuwa anaamini nchi yake na Urusi zinaweza kukamilisha makubaliano ya ujenzi wa kinu cha nyuklia nchini Iran.

Putin: Mkataba utaongeza msukumo

''Kwa mpango wa kina wa ushirikiano wa kimkakati ambao umesainiwa leo, baada ya miaka ya maandalizi, tutaweza kuimarisha uhusiano wetu katika nyanja zote ikiwemo usalama, uchumi, utamaduni na biashara, na kuimarisha pamoja uhusiano wetu,'' alifafanua Pezeshkian.

Baada ya kusaini mkataba huo, Rais Putin amesema nchi hizo mbili zilizowekewa vikwazo vikali, zimeungana katika kuupeleka uhusiano wao kwenye ngazi mpya. Akizungumza wakati akimkaribisha Pezeshkian, amesema mkataba huo mpya utaongeza "msukumo" katika uhusiano wao, karibu katika nyanja zote wanazoshirikiana. Putin amesema wanauchukulia uhusiano wao kuwa muhimu, nyeti na wa kimkakati, na wako kwenye njia hiyo pamoja wakiwa na nguvu.

''Hatutakuwa tu na fursa ya kujadiliana maeneo yote ya ushirikiano wetu, lakini pia tutasaini makubaliano ya kimsingi kati ya Urusi na Iran kuhusu ushirikiano wa kina wa kimkakati,'' alibainisha Putin.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amekutana pia na Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian amekutana pia na Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail MishustinPicha: ALEXANDER ASTAFYEV/AFP

Hata hivyo, maelezo kuhusu nyaraka za mkataba huo bado hazijatolewa, lakini Kremlin imesema utaimarisha uhusiano wa kijeshi, kisiasa na kiuchumi wa Iran na Urusi.

Kabla ya mazungumzo ya Putin na Pezeshkian, Kremlin ilipongeza kukua kwa uhusiano na Iran, ambao umeimarika huku nchi zote mbili zikijikuta zimeandamwa na vikwazo ambavyo vimewekwa na serikali za Magharibi. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema Iran ni mshirika muhimu wa Urusi, ambaye wanaendeleza ushirikiano wa pande nyingi.

Ziara imefanyika kabla kuapishwa Trump

Ziara ya Pezeshkian inafanyika siku chache kabla ya kuapishwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump Jumatatu ijayo ya Januari 20, ambaye ameahidi kuwa mpatanishi wa amani nchini Ukraine, na kuchukua msimamo mkali zaidi kuhusu Iran, ambayo inakabiliana na ongezeko la matatizo ya kiuchumi na changamoto nyinginezo, ikiwemo vikwazo vya kijeshi katika nyanja yake ya ushawishi kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Iran tayari imeshaipatia Urusi droni chapa ''Shahed'' ambazo kulingana na maafisa wa Ukraine na nchi za Magharibi, Urusi inazitumia kuishambulia Ukraine katika mashambulizi ya usiku. Nchi hizo mbili zimekuwa zikiufanyia kazi mkataba huo mpya kwa miaka mingi. Uhusiano wa sasa unaongozwa na hati ya mwaka 2001 ambayo wamekuwa wakiiongeza mara kwa mara.

(AFP, AP, Reuters)