1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marco Reus atozwa faini kubwa

19 Desemba 2014

Mchezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Marco Reus ametozwa mojawapo ya faini kubwa zaidi ya kuendesha gari kuwahi kushuhudiwa katika historia ya Ujerumani baada ya kutumia gari lake bila leseni halali.

https://p.dw.com/p/1E7iE
Marco Reus
Picha: Getty Images/M. Rose

Tukio hilo linaukamilisha mwaka ambao umekuwa mgumu sana kwa nyota huyo wa Borussia Dortmund. Mambo yalifichuka mnamo Machi 18 mwaka huu, kwa mujibu wa gazeti la michezo hapa Ujerumani “Bild“. Reus alisimamishwa na polisi wakati akiendesha gari lake aina ya Aston Martin mjini Dortmund. Alikuwa tu na kitambulisho lakini bila leseni ya kuendesha gari. Baada ya upelelezi wa polisi, ilibainika hakuwa na cheti halali cha kuendesha gari.

Sasa ametozwa faini ya euro 540,000 kutokana na makosa sita aliyokutwa nayo ikiwa ni pamoja na kuendesha gari kwa kasi katika sehemu kusikostahili.

Mchezaji huyo wa Dortmund mwenye umri wa miaka 25, anayepigiwa upatu kuwa wachezaji maarufu wenye vipaji katika timu ya taifa ya Ujerumani, alikosa kushiriki katika dimba la Kombe la Dunia kutokana na jeraha. Tangu wakati huo, amekuwa na mksimu mbovu kutokana na matatizo ya kila mara ya jeraha.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu