Marehemu rais Umaru YarÁdua wa Nigeria azikwa leo
6 Mei 2010Goodluck Jonathan mwenye umri wa miaka 52 leo ameapishwa rais mpya wa Nigeria, nchi iliyo na wakaazi wengi kabisa barani Afrika na inayokabiliwa na mivutano ya kidini na kisiasa. Baada ya kupokea madaraka yake mapya, Jonathan aliahidi kufanya marekebisho katika utaratibu wa uchaguzi ujao na kupiga vita ulaji rushwa na akaongezea:
"Hata jitahada za kuendeleza amani na maendeleo katika Niger Delta na juhudi za kulinda maisha na milki kote nchini ni kipaumbele."
Jonathan tayari alikuwa akiongoza shughuli za serikali kama rais wa mpito na hakuna mabadiliko makubwa yanayotazamiwa katika sera za serikali. Kwani YarÁdua alitoweka kwenye jukwaa la kisiasa tangu Novemba mwaka jana alipokwenda Saudi Arabia kwa matibabu ya moyo. Alirejea Nigeria mwezi wa Februari lakini hali yake ya afya haikumruhusu kufanya kazi na hakuonekana tena hadharani.
Jonathan alieshika madaraka miezi mitatu iliyopita, ameshafanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na amewateua washauri wake tangu wakati huo. Sasa atamteua makamu wa rais na serikali hiyo inatazamiwa kubakia madarakani hadi muhula wa rais uliobaki utakapomalizika mwakani na uchaguzi kuitishwa mwezi wa Aprili. Haijulikani iwapo Jonathan anaetokea Niger Delta atagombea urais katika uchaguzi ujao. Kwani katika chama tawala, kuna makubaliano yasio ya kimaandishi, kuwa wadhifa huo unakwenda kwa zamu, kati ya kaskazini na kusini. Na muhula ujao wa miaka minne ni zamu ya Waislamu wa kaskazini. Suala muhimu ni nani atakaekuwa makamu mpya wa rais. Huyo huenda akatokea kaskazini na ndie atakaegombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2011.
Marehemu YarÁdua alieahidi kuheshimu utawala wa kisheria aliposhika madaraka, alitoa matumaini kwa wananchi wengi, baada ya kumalizika utawala wa miaka minane wa rais wa zamani Olusegun Obasanjo, aliekuwa kiongozi wa kijeshi hapo awali na aliependa kupuuza amri za mahakama na kanuni zake. YarÁdua alishinda uchaguzi uliofanywa Aprili mwaka 2007 na kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo kupata uhuru wake katika mwaka 1960, serikali za kiraia zilipokezana madaraka.
Maiti ya marehemu YarÁdua imepelekwa mji wa Katsina alikozaliwa na anazikwa huko hii leo. Maelfu ya watu wamekusanyika uwanja wa ndege na wengine wamepangana barabarani. Mkaazi mmoja wa Katsina amesema,kifo cha rais YarÁdua ni hasara kubwa kwa demokrasia, kwa Nigeria na bara zima la Afrika.
Mwandishi: P.Martin/RTRE/AFPE
Mhariri: M.Abdul-Rahman