Marekani: Aliyekuwa mshauri wa usalama akiri kusema uongo
2 Desemba 2017Flynn amekiri makosa yanayohusiana na uchunguzi unaofanywa juu ya uchaguzi wa rais unaoongozwa na mwanasheria maalum Robert Mueller. Fylnn amekubali kushirikiana na mwanasheria huyo maalum anaye endesha uchunguzi hasa kuhusu kujiingiza kwa Urusi katika uchaguzi wa rais uliofanyika Marekani mwaka jana wa 2016 na pia kuhusu ushirikiano baina ya Urusi na kikosi cha Trump wakati wa kampeni zan kugombea urais.
Hatua hiyo ya Flynn inaweza kuwa ni kitisho kwa ikulu ya rais Trump ambayo katika kipindi cha mwaka uliopita kutokana kuandamawa na shughuli za uchunguzi,. Waendesha mashitaka wanachunguza tuhuma kuhusu Urusi kujiingiza kwenye kampeni za uchaguzi wa Marekani au kuhusika na kushawishi ushindi wa rais Trump.
Mshauri huyo wa zamani wa usalama ameeleza pia kwamba washirika wa karibu wa rais Trump walihusika na hata mara nyingine walitoa maagizo juu ya mawasiliano yake. Kwa mujibu wa mwanasheria maalum, mshauri huyo wa zamani wa masuala ya usalama wa Rais wa Marekani, Donald Trump,ameitaja timu ya mpito ya rais huyo kwamba ndiyo iliyomwamuru awasiliane na Urusi kabla ya utawala mpya kuingia madarakani. Madai hayo yanapingana na kauli za ikulu kwamba Michael Flynn alikuwa anachukua hatua peke yake na kwamba aliwadanganya wakuu wake juu ya mikutano yake na aliyekuwa balozi wa Urusi nchini Marekani wakati huo Sergey Kislyak. Fylnn alikutana na balozi huyo wa Urusi ili kuzungumzia juu ya vikwazo dhidi ya Urusi vilivyokuwa vimewekwa na utawala wa Obama pamoja na kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi kwenye maeneo ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa taarifa za kidiplomasia zinasema kwamba Flynn na mshauri wam rais Donald Trump ambaye pia ni mkwewe Jared Kushner walizungumzza nchi nyinginezo sio Urusi peke yake. Mwanadiplomasia mmoja ambaye hakutaka atajwe amefahamisha kwamba Jared Kushner pia alishikilia nafasi ya juu katika timu ya mpito wakati wa kampeni za kugombea urais.Flynn amedai kwamba Kushner alizungumza na Kim Darroch balozi wa Uingereza nchini Marekani
Flynn aliachishwa kazi na rais Trump kwa sababu ya kumpotosha Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence juu ya mazungumzo yake na upande wa Urusi. Bwana Pence ndiye aliyeiongoza timu hiyo ya mpito. Ikulu ya Marekani imesema madai ya Flynn hayamuhusishi mtu yeyote katika utawala wa rais Trump, na kwamba yale yanayo endelea ni hatua zinazoelekea katika kuuhitimisha uchunguzi huo unaoihusisha Urusi. Kwa mujibu wa wakili wa ikulu Ty Cobb taarifa za uongo za Flynn ndio chanzo cha kuwapotosha maafisa wa ikulu na hilo ndilo lililosababisha kujiuzulu kwake mnamo mwezi Februari mwaka huu.
Iwapo itabainika kwamba Trump alimtuma Flynn kuwasiliana na viongozi wa Urusi, jambo ambalo sio hatia kisheria lakini hata hivyo ikiwa itabainika kuwa Trump alimtaka Flynn awadanganye maafisa wa FBI kuhusu mawasiliano yake, hilo linaweza kuwa kosa la jinai limeripoti shirika la habari la Reuters.
Kiongozi wa bunge wa chama cha Democtarts Nancy Pelosi amesema hatua ya Flynn kukiri makosa hayo imesababisha giza katika historia ya Marekani. Pelosi amesema Wamarekani wote wanapaswa kuwa na hofu na taarifa juu ya jitihada za Rais Trump za kumzuia mwanasheria maalum pamoja na kuudumaza uchunguzi anaofanya. Watu wa Marekani wanastahili kukijua kile rais Trump anachojua kuhusu Urusi na suala zima la kuingilia kati katika uchaguzi wa Marekani. Bi Pelosi anauliza kwa nini Trump hataki kuichukulia hatua Urusi?.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE/p.dw.com/p/2ocb0
Mhariri: