Marekani inapima uwezo wake katika mazungumzo ya Mashariki ya Kati
4 Aprili 2014Akizungumza wakati alipokuwa Morocco baada ya mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati,kutopiga hatua kwa wiki nzima, Waziri Kerry alisema kuna viwango vya juhudi za Marekani iwapo pande husika hazitokuwa na nia ya kusonga mbele katika mazungumzo hayo.
Waziri huyo ambaye alikuwa akizungumza na waandishi habari mjini Rabat Kerry amesema kwa sasa ni lazima Marekani ijadili kwa kina hatua muhimu zitakazopigwa huku akisema anasafiri mjini Washington leo kujadili suala hilo na rais Barrack Obama.
Kerry amesema kwa sasa anaziomba pande zote mbili, Israel na Palestina kujitolea kwa ukamilifu kufanikisha mazungumzo ya amani.
Matamshi haya yamekuja baada ya matukio ya kulipizana kisasi kati ya Palestina na Israel wiki iliopita yaliovuruga kabisa mazungumzo hayo yaliovaliwa njuga na Marekani. Pigo la kwanza lilitokeani pale Israel iliposhindwa kuwaachia wafungwa wa mwisho kama ilivyotarajiwa kufanyika mwishoni mwa juma.
Baadaye siku ya Jumanne Palestina nayo ikatuma ombi la kujiunga na Mashirika ya Kimataifa 15 yanayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, Hatua ambayo iliikasirisha Israel iliosema jambo hilo linakiuka matakwa yaliokubalika katika kuyafufua mazungumzo mnamo Julai iliopita.
Aidha Kiongozi wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmood Abbas, ametupilia mbali ombi la John Kerry kutaka Palestina kusimamisha ombi lao.
Marekani bado inamajukumu makubwa ya kutuliza migogoro duniani
Hata hivyo Waziri John Kerry amesema, Marekani ina masuala mengi inayoyashughulikia akigusia majadiliano na Urusi juu ya Ukraine, Majadiliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, na hata mgogoro wa Syria miongoni mwa mambo mengine.
Akizungumzia mgogoro wa Mashariki ya Kati, Kerry amesema mpaka sasa hakuna upande wowote uliojitoa katika mazungumzo lakini akasema hawawezi kukaa katika meza ya mazungumzo milele.
Kwa upande wake afisa wa ngazi ya juu wa Israel Nabil Shaath, aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa Kiongozi wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmood Abbas, hana nia ya kumkasirisha John Kerry bali kuikumbusha Israel juu ya kushindwa kwake kuwaachia wafungwa.
Nabil Shaat amesema bado wataendelea na mazungumzo lakini anatumai subira ya Marekani itamalizika kwa sababu ya hatua za Israel wala sio Palestina.
Mwandishi Amina Abubakar/Reuters/AFP
Mhariri Mohammed Abdul-Rahman